Na: Meshack Maganga-Mjengwablog,Iringa.
Kwa muda mrefu sasa nimejijengea utamaduni imara wa kujisomea vitabu. Sisomi kila aina ya vitabu, isipokuwa ninapenda sana vitabu vya biashara na uchumi (finances, economic, entrepreneurship and business) pili ni vile vya mahamasisho na shuhuda (motivational and inspirational) na vingine ni vile vinavyohusu ustawi wa kiroho na kimaisha (spiritual and personal improvements). Mara chache sana huwa navisoma vitabu vinavyohusu siasa.
Nimejiwekea ratiba ya kusoma angalau vitabu viwili kila mwezi ambayo ni idadi ya vitabu ishirini na nne kwa mwaka. Pia ni msikilizaji mzuri wa rekodi za sauti zenye maudhui kama ya vitabu nilivyovitaja. Pamoja na kusoma kote huku vitabu huwa nina mchujo mkali sana wa vitabu vya kusoma kutegemea na sifa za mwandishi husika.
Daima huwa nasoma kazi za waandishi ambao wamepitia kwa vitendo waliyoyaandika na sio wale wanaoandika nadharia. Sisomi kazi za wenye vyeti vikubwa vya madarasani, ninasoma kazi za wenye uzoefu kwa yale waliyoyaandika kivitendo.
Ndio maana ninapenda sana vitabu kama ‘Retire Young Retire Rich’ (Robert Kiyosaki), ‘As A man Thinketh’ (Allen James), ‘Secrets of Millionaire Minds’ (Harv Eker), ‘Think and grow rich’ (Napoleon Hill) “Financial IQ” (Robert Kiyosaki), kwa kuvitaja kwa uchache. Nawapenda waandishi hawa kwa sababu wameandika kile walichokiishi. Huu ni mtazamo na msimamo wangu. (usijichoshe kuuhoji wala kuukosoa)
Ndio maana kila siku ninapojiuliza ni kwa nini tunazalisha wasomi wengi wenye vyeti katika maarifa ya biashara lakini hatuoni wakitumia elimu zao kuibua miradi, biashara na kutengeneza ajira; ninabaini kuwa moja kwa moja tatizo lipo kwenye mifumo yetu ya kielimu.
Ni vigumu sana profesa (ama mhadhiri) anaefundisha kozi ya biashara chuo kikuu (ambaye hana hata banda la kuuzia chipsi) kuzalisha mjasiriamali/mfanyabiashara halisi. Anachoweza kufanya ni kuzalisha wenye vyeti wengi ambao wanabaki kuwa mzigo mitaani. Kama ambavyo huwezi kujifunza kuogelea kwa kusoma maandishi, pia haiwezekani kujifunza biashara kwa kusoma vitabuni pekee.
Kama inavyotakiwa kuingia majini na kuanza kugusa maji, ndivyo ilivyo hata kwa biashara, ni lazima uingie na kuionja. Mkufunzi wa uogeleaji atafanikiwa kuzalisha waogeleaji wengi na walio mahiri kwa kuonesha kwa vitendo namna ya kuogelea (ikiwemo upigaji mikono na urushaji miguu ukiwa majini).
Ndivyo ilivyo pia kwa wasomi wakufunzi wa mambo ya biashara na ujasiriamali. Hatuwezi kuzalisha wajasiriamali wa ‘ukweli’ ikiwa wanaowafundisha hawajawa mifano ya kuigwa (they are not role models). Hali hii tete inaibua tatizo jingine kubwa katika ujasiriamali wa kitanzania pale zinapohitajika huduma za kitaalamu ikiwemo ushauri wa kibiashara.
Kiukweli ushauri wa kitaalamu katika ujasiriamali na biashara unahitajika sana hasa katika nyakati hizi ambazo tunapambana na ushindani wa kimataifa. Unaposikia neno ushauri pamoja na mantiki yake ni kwamba huwa una machaguo matatu. Unaweza kuukataa wote, unaweza kuutumia wote ama ukachukua kidogo na kuikataa sehemu fulani. Yote katika yote ushauri wa kibiashara tunatazamia unapotumika ulete tija ya uboreshaji wa biashara ama eneo uliloshauriwa.
Biashara zinahitaji kuwa na michanganuo ya kitaalamu ambayo husaidia kukupa dira ya namna ya kutekeleza malengo yako. Michanganuo huweza kutoa mwangaza wa kujua ni wapi hapaendi sawa na mbinu gani zitumike kuokoa hali pale mambo yanapoenda hali jojo. Maeneo mengine yanayohitaji utaalamu ni katika uibuaji wa biashara mpya, utunzaji wa hesabu, uratibu wa masoko pamoja na upatikanaji wa mikopo na mienendo ya kodi.
Ukiniomba mimi nikushauri masuala ya biashara sitakuja na mwarobaini wa mafanikio yako (tena hakuna yeyote mwenye mwarobaini wa mafanikio yako). Nitakachofanya mimi ni kukushauri mbinu za kiujumla na siri za kufanya biashara. Lakini ukitaka tija zaidi nitakupa wazo jingine.
Kwa mfano; kama wewe ni mfanyabiashara wa huduma za daladala ama unakusudia kuanzisha biashara hiyo ni vema ukamtafuta mfanyabiashara mzoefu katika eneo hilo la daladala ili akupe ‘specific’ mbinu na mazingira halisi. Huyu kwako mimi ninamhesabu ni mtaalamu wako. Itakuwa ni bahati tu inapotokea umeniomba ushauri wa kibiashara halafu ikawa kuwa biashara unazofanya ama kukusudia kufanya ni zile ambazo mimi pia ninazifanya.
Maana yangu hapa ni kuwa, utaalamu katika biashara upo wa aina mbili. Kuna wale waliokaa darasani na kufundishwa biashara (bila kujali ikiwa wanafanya ama hawafanyi biashara) na wengine ni wale ambao licha ya kutoingia darasani, wanauzoefu mkubwa wa kibiashara. Hawa wote ni vema kuwatumia kwa kadiri ya mazingira na mahitaji yako kibiashara.
Unapotafuta mtaalamu wa kukushauri (ikiwa unataka msomi) mimi ninadhani ni vema kuwapata wataalamu ambao wana uzoefu wa kivitendo katika biashara mbalimbali.Robert Kiyosaki, katika kitabu chake cha “Guide to Investing” anashauri kuwa “ukitaka kwenda kupanda mlima Evarest, ni vizuri ukamuuliza mtu aliyewahi kupanda mlima Evaresti”. Mimi ninaongeza hapa kwa kusema, ukitaka kwenda hifadhi ya Ruaha, muulize mtu aliyewahi kwenda huko. Pia katika biashara ni vizuri kupata ushauri kwa wafanya biashara walio ktika biashara.
Najua hii ni changamoto kubwa kwa sababu wasomi wengi wa mambo ya biashara hawafanyi biashara, lakini kwa kuwa tunao wasomi wachache wa biashara ambao wanafanya biashara ni vema kuwatumia hao. Bila kuwa makini unaweza kupotezwa kwa sababu ‘wataalamu’ wengi hutumia muda mwingi kueleza namna mambo yasivyowezekana.
Hata hivyo katika ufanyaji biashara, ni vema sana kuachana na mazoea ya kufanya biashara kienyeji, badala yake kuna umuhimu wa kuingiza utaalamu katika ujasiriamali wetu. Hii itasaidia sana kuratibu mafanikio yako na kuachana na hesabu za kubahatisha kwa kwenda kwa kupapasa.Tunapaswa kuwatumia wataalamu washindi katika biashara zetu.
meshackmaganga@gmail.com
|