Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Edward
Lowassa
Wabunge wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi
na Usalama (NUU) ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wameanza ziara yao ya kikazi na mafunzo hapa Umoja wa Mataifa.
New York
Mwandishi maalum wa www.francisgodwin.blogspot.com kutoka New York anaripoti kuwa ,Wabunge hao watano wakiongozwa na mwenyekiti wa Kamati, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa ( Mb), waliwasili Jijini New York siku ya Alhamisi, ambapo siku ya Ijumaa walianza ziara yao kwa kuutembelea Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Wabunge hao ni Mhe. Beatrice Shelukindo, Mhe. Rachel Masishanga, Mhe. Khalifa Khalifa na Mhe. Vita Kawawa.
Akielezea madhumuni ya ziara hiyo, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mwenyekiti wa Kamati. Mhe. Beatrice Shelukindo aliwaeleza maafisa wa Ubalozi kwamba, ziara yao ilikuwa inalenga pamoja na mambo mengine, kujifunza na kupata uelewa wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Balozi za Tanzania nje ya nchi.
Aidha akasema ziara hii ni ya kwanza ya aina yake kufanywa na kamati hiyo na kwamba itawapa fursa ya, siyo tu kufahamu kazi zinazofanywa na Balozi, lakini pia namna bora ya kuishauri serikali hususani katika kuangalia ni kwa namna gani bora zaidi ambapo balozi za Tanzania zinaweza kuchangia katika kukuza pato la taifa, lakini pia kutekeleza kwa ufanisi na tija sera ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi.
Halikadhalika wabunge hao, kupitia ziara hiyo wanataka kujifunza mafanikio ya yatokanayo na kazi za kila siku zinazofanywa na Balozi hizo, changamoto wanazokabiliana nazo, na maeneo gani yanayotakiwa kutiliwa mkazo au kutafutiwa ufumbuzi.
Wabunge wakiwa hapa New York watapata pia fursa ya kutembelea na kukagua majengo yanayomilikiwa na serikali
Wakiwa ubalozini hapa, walipata fursa ya kuwasikiliza maafisa wa Ubalozi wanaosimamia Kamati Sita za Balaza Kuu la Umoja wa Mataifa. Wakiongozwa na Kaimu Balozi, Dkt. Justin Seruhere kila mmoja alitoa muhtasari wa kamati anayoifanyia kazi, akielezea mafanikio na changamoto wanazokabiliana zao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge hao pia walipata fursa ya kwenda Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo walihudhuria majadiliano ya mikutano miwili mikubwa inayoendelea kwa sasa hapa Umoja wa Mataifa.
Mikutano waliyohudhuria wabunge hao ni ule wa mchakato wa maandalizi ya Mkataba wa Biashara ya Silaha ( ATT), na Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na Masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC). Mikutano hii imeanza mwanzoni mwa wiki hii.
Wakiwa katika ukumbi wa mkutano wa majaliano ya ATT, wabunge waliweza kujionea na kufuatilia namna ambavyo majadiliano yalivyokuwa yakifanyika, huku kila nchi ilivyokuwa ikiwasilisha hoja huku zikiteteza misimamo na maslahi ya nchi zao.
Mkutano wa nchi wanachama kuhusu Mkataba wa Biashara ya Silaha Duniani, ambao Tanzania inashiriki kikamilifu na kufuatilia kwa karibu masuala ya udhibiti wa silaha ndogo ndogo na za kati . Silaha ambazo zimekuwa na madhara mkubwa kwa maisha na uhai wa watu barani Afrika.
Mkutano huu ambao ni na nyeti dhumuni na lengo lake kuu ni kuandaa Mkataba wa kisheria utakaoratibu na kudhibiti biashara ya silaha Duniani.
Tanzania katika mkutano huu ukiacha maafisa wa ubalozi, inawakilishwa na ujumbe mzito wa wataalamu kutoka, Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao ni Brigedia Generali Dkt. Charles Muzanila, na Brigedia Generali Venance Mabeyo, kutoka Jeshi la Polisi ni Kamishina Msaidizi, Esaka Mugasa, Bw. Theobald Kazora kutoka Ofisi ya Rais ( Ikulu) na Bw. John Kinuno, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa Upande wa Mkutano wa katika mkutano wa ECOSOC ambao ajenda yake kuu ni uhuishaji na uchagiaji wa ajira kwa vijana ujumbe wake unaongozwa na Mhe. Gaudentia Kabaka(Mb) Waziri wa Kazi na Ajira, ujumbe ambao unaojumuisha pia wawakilishi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
|
No comments:
Post a Comment