Monday, April 22, 2013

DOGO ATENGENEZA HELIKOPTA KENYA... AONYWA KUIPAISHA!!

Onesmus Mwangi, 20, akiwa na maafisa usalama kijijini kwao, nyuma ni Helikopta aliyotengeneza na kusema yuko mbioni kuirusha.
 
Kijana mmoja Onesmus Mwangi, 20, ambaye ametengeneza helikopta kwa kutumia vyuma chakavu na plastiki katika eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu nchini Kenya ametahadharishwa dhidi ya kujaribu kuipaisha angani bila kibali cha wakuu wanaohusika.

Naibu wa kamishna wa polisi wa Githunguri, Bw Fredrick Ndunga amesema utaratibu unaostahili lazima ufuatwe kwa mtu yeyote anayejitokeza na ugunduzi wa kitu chochote.

Ndunga ameonya kuwa haitaruhusu watu kufanya majaribio hatari ambayo  yanaweza kudhuru maisha ya watu.

Ndunga alitoa tahadhari hiyo afisini kwake jana baada ya kijana huyo kuwashangaza wakazi wa eneo hilo aliposema kuwa yuko karibu kuendesha ndege yake ambayo imemchukua miezi saba kutengeneza.

Thursday, April 18, 2013

Uchapishaji pasipoti wasimama

Uchapisha wa Hati za Kusafiria (Pasipoti), nchini umesimama kwa muda baada ya mashine zinazotumika kuharibika, Mwananchi limebaini.


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na baadaye kuthibitishwa na Idara ya Uhamiaji, umeonyesha kuwa tatizo hilo lilianza Januari na litaendelea hadi Mei mwaka huu.
Kusitishwa kwa huduma hiyo kumesababisha mrundikano wa maombi ya hati hizo. Waombaji wanaopigwa kalenda kupata hati hizo ni pamoja na wanaoomba kwa mara ya kwanza na wale wanaotaka mpya baada ya za awali kujaa au kumalizika muda wake.
Kabla ya mashine hiyo kuharibika muombaji aliweza kupata pasipoti yake ndani ya siku saba, baada ya kukamilisha taratibu za uombaji, lakini kutokana na tatizo hilo, imetimia miezi mitatu sasa, waombaji hawajui watapata lini hati hizo.
Baadhi ya waombaji walioongea na gezeti hili walilalamikia kitendo hicho wakisema kinawasababishia usumbufu na kuwakwamisha katika kufanya.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji na vishoka, tayari wameanza kujinufaisha na tatizo hilo kwa kuomba rushwa kutoka kwa waombaji hati hizo ili wawatekelezee matakwa yao kwa haraka.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mbarak Abduwakil alikataa kuzungumzia suala hilo, akidai kuwa amebanwa na vikao ofisini kwake.Hata hivyo, Kaimu Ofisa Uhusiano wa Uhamiaji, Tatu Burhan alikiri kuwepo kwa tatizo hilo, lakini akasema halitokani na mashine zao kuharibika.
"Tatizo hili limetokana na ukosefu wa malighafi toka nje ya nchi. Unajua malighafi hizo tunaziagiza, lakini kwa bahati mbaya hazikuweza kupatikana kwa wakati," alisema Tatu.
Pamoja na uhaba wa mali ghafi, alisema kwa bado Uhamiaji iliendelea kutoa pasipoti kwa wenye maombi maalumu ya dharura.Alikiri pia kwamba kwa waombaji wasio na dharura maombi yao yaliwekwa kando yakisubiri kuwasili kwa malighafi.
Hata hivyo Tatu alisema kuwa mali ghafi hizo zimeshawasili Bandari ya Dar es Salaam jana na walikuwa katika harakati za kuzitoa.
"Hivi ninavyozungumza (jana) malighafi ghafi hizo tayari zimefika bandarani na tupo kwenye harakati za kuzichukua," alisema.
Alisema kuwa pamoja na malighafi hizo kuwasili ni vigumu kuchapisha pasipoti zote kwa wakati mmoja kutokana na wingi wa maombi.CHANZO MWANANCHI

Watoto 2 wasombwa na mafuriko Kenya

Polisi nchini Kenya wameelezea BBC kuwa watoto 2i wamekwama nyumbani kwao baada ya kufukiwa na tope na maji yaliyosababisha maporomoko ya ardhi.

Watoto hao walikuwa wamelala katika kijiji cha Narok kilomita kadhaa kutoka mji wa Nairobi, mvua kubwa iliponyesha na kusababisha maji kusomba majumba kadhaa katika mtaa wao.

Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya limeonya watu wanaoishi maeneo yanayotishiwa kukumbwa na mafuriko wahamie sehemu za juu na milima.

Mvua kubwa imekuwa ikinyesha katika sehemu nyingi nchini humo na inaaminiwa kuendelea kunyesha.

Katibu mkuu wa shirika hilo nchini Kenya Abbas Gulet ameambia BBC kuwa maeneo yaliyoahiriwa zaidi ni pamoja na Nairobi na maeneo yaliyo pembezoni, na garissa ambapo watu kadhaa wamefukiwa na maporomoko ya ardhi au kuzingirwa na maji.

Maafa makubwa

Kufikia sasa watu 36 wamefariki kutokana na mafuriko hayo yaliyoanza chini ya mwezi mmoja.

Kawaida msimu wa mvua nchini Kenya huwa kati ya mwezi Machi na May, lakini wadadisi wanasema kuwa safari hii mvua imenyesha kwa wingi zaidi.

Mwimbaji Bi Kidude aaga Dunia Zanzibar


Mwimbaji Bi Kidude aaga Dunia Zanzibar


Mwimbaji nguli wa muziki wa tarabu nchini Tanzania Fatma binti Baraka, maarufu kama Bi Kidude amefariki Jumatano kisiwani Zanzibar akiwa na umri wa zaidi ya miaka 100.
Taarifa ya kifo chake ilitolewa na mjukuu wake Fatuma Baraka ambaye pia ni muimbaji wa Taraabu. Alisema Bi Kidude alifariki hospitalini kutokana na maradhi ya kisukari na uvimbe kwenye Kongosho.
Bi Kidude amekuwa katika fani ya muziki wa taarab ya kiasili pamoja na ngoma za unyago kwa zaidi ya robo tatu ya umri wake.
Katika miaka ya karibuni afya yake imekuwa ikizorota kiasi cha serikali ya Zanzibar kumzuia kupanda majukwaani kuburudisha japokuwa alionekana katika tamasha la Sauti za Busara mwezi Februari mwaka huu.
Mipango ya mazishi ya nguli huyu inafanywa nyumbani kwake Zanzibar.
Wengi, hasa vijana wa kizazi kipya wanamfahamu Bi. Kidude kwa uwezo wake mkubwa wa kuimba taarabu kwa kuchanganya lugha ya kiswahili na ile ya kiarabu. Nyimbo zake za kiarabu mara nyingi zimekuwa na ladha kama ile ya aliyekuwa mwimbaji gwiji wa Misri Ummu Kulthumu.
Sio uimbaji tu uliomfikisha Bi. Kidude alipofika, bali uwezo wake pia wa kutunga mashairi, kutumia ala za mziki kama vile kupiga ngoma na hata ngoma za unyago, vyote hivi vilimuweka Bi. Kidude katika nafasi tofauti katika jamii.
Alikuwa na tabia ya kumwita kila mtu 'mwanangu,' ingawa yeye mwenyewe hakubahatika kupata mtoto. Katika mahojiano aliyofanyiwa na vyombo mbali mbali vya habari, mwenyewe alisikika akisema, ingawa alikuwa na hamu ya kupata mtoto, lakini Mwenyezi Mungu hakumjaalia.
Katika miaka ya hivi karibuni, Bi. Kidude alishirikishwa sana na wasanii wengine katika kazi zao. Miongoni mwao ni Ahmada Amelewa, Fid Q Juhudi za Wasiojiweza.
Mbali na hayo, mashirika mbali mbali yakiwemo ya kibiashara na yale yasiyo ya kiserikali yaliona mvuto aliokuwa nao Bi. Kidude katika jamii, hivyo wakamtumia katika matangazo mbali mbali maarufu likiwa lile la kutokemeza Malaria.
Ni bibi aliyebahatika kusafiri takriban duniani kote, na vilevile katika maisha yake alijinyakulia tuzo lukuki. Miongoni mwa hizo ni ile ya 2005 WOMEX ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki.
Katika siku zake za mwisho, Bi. Kidude alikuwa akiumwa, lakini wengi wanahusisha kuumwa kwake na utu uzima aliokuwa nao.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa wote, lakini zaidi ni wanamziki wa kizazi kipya waliokuwa wakimuona Bi. Kidude ni nyanya yao.

CHANZO: BBC


Wednesday, April 17, 2013

Bungeni kwachafuka: Wabunge watano watolewa nje

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi (kulia) akizungumza na wabunge wa Chadema baada ya kikao cha kunge kualishwa jana mchana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Dodoma.Wabunge watano wa Chadema jana walitimuliwa bungeni na kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano kutokana na vurugu zilizotokea jana usiku.

Wabunge hao ni Lissu, Hezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).

Chanzo za kufukuzwa kwao ni kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba.

Kutokana na tafrani hiyo, Nchemba hakuweza kuhitimisha hotuba yake hivyo Ndugai alilazimika kukatisha mkutano wa Bunge.Hata hivyo wakati akiahirisha mkutano huo, tayari wabunge hao walikuwa wameshatolewa nje baada ya askari kuongezwa.

Mapema Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alitoa tusi zito la nguoni wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, licha ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kupiga mkwara wa kuwashughulikia wabunge watakaorusha matusi.

Mbali na tukio hilo Lema naye alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu viongozi wa CCM akiwamo Rais Jakaya Kikwete kwa udini, madai ambayo Bunge limempa siku saba kuyathibitisha.

Lema aliituhumu CCM na Serikali yake chini ya Rais Kikwete kwa kushindwa kutatua mgogoro wa kidini na badala yake kuwa kama analikwepa tatizo. Alionya kuwa Taifa linapasuka kwa migogoro kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa kulishughulikia.

Kauli iliwanyanyua vitini Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu na Sera), William Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Lukuvi na Jaji Werema walisimama wakidai kuwa Lema alikuwa amemdhihaki Rais Kikwete kwa kauli zake za kumhusisha na masuala ya udini.

Hata hivyo, Mnadhimu Mkuu wa Upinzani, Lissu alisimama kumtetea Lema akidai hakuwa amemdhihaki Rais bali alikuwa amemkosoa kitu ambacho kanuni za Bunge zinaruhusu.

Lema aliruhusiwa kuendelea na hoja yake na ndipo akamtolea mfano Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira wakati alipokwenda Mwanza kutatua mgogoro baina ya Wakristo na Waislamu kuhusu suala la kuchinja.

“Wassira akifahamu yeye ndiye, Waziri alikwenda Mwanza na kuwaacha viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu watatue wenyewe suala la kuchinja. Sasa alitaka diwani atatue mgogoro ule?”

Baada ya kumaliza kuchangia, Naibu Spika alitangaza kuwa Lema anatakiwa kuwasilisha katika muda wa siku saba uthibitisho kuwa Rais anahusika na tatizo la udini.

Chanzo: Mwananchi

SAD:DENTI AJICHOMA MOTO BAADA YA KUPOTEZA ADA!!

.....Pichani Emmanuel akipatiwa matibabu kutokana na majeraha ya moto aliyopata.
Mwanafunzi wa shule ya ufundi ya Nsambya nchini Uganda amejichoma moto baada ya kupoteza ada ya shule aliyopewa na baba yake.

Mwanafunzi huyo Emmanuel Ogabe, mtoto wa Bw. Moses Ogabe hivi sasa anatibiwa majeraha hayo ya moto katika hospitali ya Mulago ambako alikimbizwa baada ya kufanya jaribio hilo la kujitoa uhai wake siku ya Jumanne usiku ambapo baba yake Mzee Ogabe amesema mtoto huyo mara kadhaa amekuwa akijaribu kujiua.

Ogabe amesema alijaribu kujitoa uhai wake kwasababu amekuwa akidai kutengwa na wazazi wake wakati wanajitahidi kumpatia mahitaji yake hivyo hakuweza kuvumilia jinsi atakavyomwangalia baba yake baada ya kupoteza shilingi laki moja za Uganda alizopatiwa na baba yake.

Amesema alipogundua kuwa amepoteza pesa hizo, kijana huyo alirejea nyumbani na kujitumbukiza ndani ya mafuta ya taa kisha kujiwasha kwa kiberiti ambapo aliokolewa na baba yake ambaye alimkimbiza na kuuzima moto huo kwa maji.

Monday, April 15, 2013

Damas: Mtunzi wa Nyamidela anayelia na ukosefu wa fedha


Na John Mnubi

“NILIANZA kugundua kuwa nina kipaji cha muziki tangu mwaka 1998 nikiwa darasa la sita huko mkoani Morogoro.”
Hayo ni maneno ya Damas Masonda anayetamba na kibao chake cha Nyamidela.
Alizaliwa mwaka 1984 mkoani Iringa katika Kijiji cha Mdabulo wilayani Mufindi, lakini akiwa na miaka mitano walihamia Morogoro kutokana na wazazi kutafuta maisha bora.
Alijiunga na elimu ya masingi mwaka 1993 ambapo mwaka 1999 alihitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Morogoro ambako aliishia kidato cha pili kutokana na wazazi kushindwa kuendelea kumsomesha.
Anasema kutokana na ugumu wa maisha, baada kuacha shule alijiingiza kwenye biashara ya uuzaji wa maembe sindano ambayo alikuwa akiyafuata mlimani Kigurunyembe akiyaweka kwenye sinia na kutembeza mitaani ili kujikimu.
Baada ya kusota na maisha magumu alipata wazo ambalo alihisi lingemfanya afanikiwe kimaisha kupitia muziki ndipo alipoanza kuchanganua ni wapi aende ili afanikiwe, akapata jibu la kwenda Mwanza ambapo angekutana na mtayarishaji wa muziki maarufu kama Kid Bway wa Tetemesha Records.
Anasema alidunduliza fedha na kupata nauli ambapo alipanda treni kuelekea Mwanza. Alifikia maeneo ya Mwaloni ambako aliweka maskani yake huku akimuulizia mtayarishaji huyo wa muziki.
Lakini nyakati za mchana, Damas alikuwa akifanya vibarua vya kuaniaka dagaa, malazi yake yalikuwa kando kando ya Ziwa Victoria, maarufu kama Mwaloni.
“Baada ya kumtafuta kwa muda wa wiki mbili nilifanikiwa kukutana na vijana wenzangu wawili wenye kundi lao liitwalo Wabuza kutoka Sengerema ambao nao walikuwa kwenye harakati kama za kwangu ambapo tulifanya wimbo mmoja na Kid Bway lakini haukufanya vizuri,” anasema Damas.

Mafanikio
“Binafsi nimewahi kutunga na kuimba nyimbo karibu 14 lakini ninazojivunia kati ya hizo ni Mautamu iliyoandaliwa na prodyuza Hassy Kiss na hivi karibuni nimeachia kibao cha Nyamidela kilichotengenezwa katika studio za Shega Records jijini Kampala, Uganda,” anasema.
Anasema wimbo huo wa Nyamidela, ambao una mchanganyiko wa lugha mbili za Kihehe na Kiswahili, umefanikiwa kukakamata chati za juu kwa wiki kadhaa mfululizo katika kituo cha Radio Ebony FM kilichopo mjini Iringa.
Aidha, alifanikiwa kutengeneza video ya wimbo wake wa Mautamu, ambayo imetengenezwa na A Touch of Kalabani Video iliyopo jijini Dar es Salaam na tayari amekwishaisambaza kwenye vituo mbali mbali vya televisheni jijini Dar es Salaam ambako inachezwa.
“Katika kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia niliamua kuuweka kwenye mtandao maarufu wa www.youtube.com wimbo wangu wa Mautamu ambao nimeufanyia video ili dudia nzima waweze kuuangalia,” anasema Damas.
Aidha, Damas amefanikiwa kukutana na wasanii na watayarishaji wengi wakubwa wa muziki kupitia sanaa anayoifanya jambo ambalo limempanua upeo na kujifunza mengi kuhusu muziki.

Nyamidela
Anasema katika wimbo wa Nyamidela, ambalo ni neno la Kihehe likimaanisha ‘Matembele’ kwa Kiswahili, kwa kiasi kikubwa ameimba kuhusu wanawake wanaojiremba na kufanya ukware na kutembea na waume za watu, hatimaye kuvunja ndoa za wenzao na kuwaasa kuachana na tabia hizo ambazo si njema katika jamii na badala yake kila mmoja abaki na wa kwake.

Changamoto
Miongoni mwa changamoto zinazomkabili Damas ni kukosa kualikwa kwenye matamasha mbali mbali hata yale madogo yanayofanyika mkoani Iringa. Anasema amekuwa akikosa morali ya kufanya vitu bora zaidi kutokana na kukosa mialiko ambayo ingemtia moyo na kumuongezea kipato cha kujikimu na maisha.
“Tangu nianze muziki sijawahi kushika pesa taslimu ambayo naweza kusema nitaiwekeza au itanisaidia kujikimu na maisha zaidi ya kuambulia umaarufu tu na kujulikana na watu wengi, basi,” anasema.
Anasema anakabiliwa na hali ngumu linapokuja suala la kusambaza kazi zake ambapo hutumia nguvu nyingi kufanikisha suala hilo kwa sababu hana msimamizi wa kazi zake, yaani meneja.
“Nashindwa kufanya video kwa sababu unakuta wimbo umekubalika redioni, lakini sina fedha mfukoni, maana fedha inahitajika ili kufanikisha hilo. Bado nalia na kukosa mialiko kwenye matamasha maana nikialikwa nitapata fedha ya kutengeneza video nzuri,” anasema.
Kutokana na kuanza kuisambaza kazi ya Nyamidela kijijini kwake Nyabula, alivamiwa na kupigwa nyundo kichwani na kulazwa miezi mitatu mwishoni mwa mwaka 2012 akidai ni tukio lililotekelezwa na baadhi ya wanakijiji wenye wivu ambao hawakupenda mafanikio yake hasa walipokuwa wakisikia kibao chake kikipigwa karibu kila kona kijijini hapo.

Matarajio yake
Mara baada ya kupata fedha anatarajia kufanya video ya wimbo wake wa Nyamidela ambapo ataifanyia mkoani Iringa ikiwa ni njia moja wapo ya kuutangaza mkoa huo, lakini pia ujumbe na lugha iliyotumika kwenye wimbo huo kuwagusa zaidi wakazi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla.

Wito
Anasema waandaaji wa matamasha mjini Iringa na Tanzania kwa ujumla waweke mkazo kuwaalika wasanii wazawa kama njia mojawapo ya kuinua vipaji vyao.
Aidha, aliwaomba wakazi wa Iringa kupenda vya kwao na kuachana na kasumba ya kupenda vitu kutoka magharibi.

Mfanyabiashara Maarufu Kilimanjaro, Arusha Aanguka na Ndege na Kufariki Dunia

Ndege aina ya Cessna 5H-QTT ikiwa imeanguka eneo la Kisongo, karibu na Uwanja wa Ndege Arusha juzi jioni, baada ya kugonga mti wakati ikijiandaa kutua na kusababisha kifo cha mmiliki wake na aliyekuwa rubani, Bob Sambeke(katika picha ndogo juu). Picha na Filbert Rweyemamu

 

 

 

 


KWA mara nyingine, Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha imetikiswa, kutokana na kifo cha mfanyabiashara maarufu katika mikoa hiyo, Joseph Sambeke (49) maarufu kama Bob Sambeke. Bob Sambeke alifariki dunia juzi jioni baada ya kuanguka na ndege ndogo aliyokuwa akiiendesha, kilomita moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Arusha wakati akitokea mkoani Kilimanjaro.

Huu ni msiba wa tatu katika muda wa mwezi mmoja kwani mwishoni mwa mwezi jana, Wakili na Mfanyabiashara maarufu mkoani Arusha, Nyaga Mawalla alifariki dunia, ikiwa ni siku moja tagu kufariki ghafla kwa mfanyabiashara mwingine wa madini wa mkoani humo, Henry Nyiti. Ndege ya Sambeke aina ya MT 7- namba 5H-QTT ilianguka saa 12.34 jioni baada ya bawa lake kugonga mti katika eneo la Magereza linalopakana na uwanja huo.

Alijeruhiwa na baadaye alifariki akiwa njiani wakati akiwahishwa hospitalini na askari wa Magereza ambao wanaishi katika kambi alipoanguka. Mazishi yake yamepangwa kufanyika Alhamisi eneo la Karanga, Moshi.

Meneja wa Uwanja wa Ndege Arusha, Ester Dede alithibitisha jana kutokea kwa ajali hiyo, na kueleza kuwa taarifa za awali zinaonyesha ndege hiyo ni mali ya marehemu Mawalla ambaye alikuwa mbia wa biashara na Bob Sambeki na imesajiliwa kupitia Kampuni ya Quality Tours & Travellers. Hata hivyo, Wakili Alex Msando, ambaye pia alikuwa mshirika wa Mawalla, aliliambia gazeti hili kuwa Sambeke alikuwa ameinunua ndege hiyo kutoka kwa marehemu.

Dede alisema ndege hiyo, ilianguka mita 200 kutoka njia namba 8 ya kuruka ndege katika uwanja huo ikitokea Kilimanjaro, katika dakika 15 za muda wa nyongeza wa matumizi ya uwanja huo. Alisema ndege hiyo ikiongozwa na rubani Bob Sambeki ina uwezo wa kubeba watu wanne akiwamo rubani. Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo, walisema kabla ya kuanguka ndege hiyo, ilikuwa ikiyumba na iligonga mti mkubwa katika moja ya mabawa yake na kupoteza mwelekeo.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Julias Laizer alisema kwamba aliona ndege hiyo ikigonga mti na kuyumba, kisha kudondoka chini na ndipo askari wa magereza walipojitokeza kutoa msaada. Laizer alisema Sambeki alikuwa peke yake na alijeruhiwa kichwani.

Kifo chake

Taarifa za kifo chake zilianza kuzagaa kwa kasi juzi saa 2:00 usiku na kusababisha taharuki katika Miji ya Moshi na Arusha.

CAG Ataka William Mhando wa Tanesco na Mkewe Washitakiwe


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amemuweka kitanzini aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, baada ya kushauri ashtakiwe pamoja na mkewe, Clara, kutokana ukiukwaji wa sheria katika kutoa zabuni.
Mbali na Mhando, wengine ambao CAG amependekeza wachukuliwe hatua za kisheria ni Mkurugenzi wa Kampuni ya McDonald Live Line Technology, watu wote walioingia katika biashara na Tanesco kinyume cha sheria pamoja na wafanyakazi waliohusika kutoa zabuni hizo.
Mapendekezo hayo ya CAG, Utouh yamo katika ripoti yake ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya 2011/12, aliyoiwasilisha bungeni wiki iliyopita ikirejea ukaguzi maalumu uliofanyika katika shirika hilo kutokana na maombi ya bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo. CAG pia ameweka wazi kuwa Tanesco iligubikwa na ukiukwaji uliokithiri wa Sheria ya Ununuzi ya 2004 na kanuni zake za mwaka 2005, uliosababishwa na viongozi wake wa juu.
“Mkurugenzi Mkuu wa Shirika akiwa ndiye mwenye uamuzi wa kuhusu ununuzi, alishindwa kuzuia ukiukwaji huu wa sheria ya ununuzi na mara nyingi aliidhinisha ununuzi wa chanzo kimoja au usiozidi ushindani,” inasema ripoti hiyo na kuongeza:
“Bodi inatakiwa kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) yale yote yaliyogunduliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kubaini kuwapo kwa rushwa na ubadhirifu.”
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa na Mhando, huku akibainisha kuwa mkewe, ambaye ni Mtendaji wa Mkuu wa Kampuni za Santa Clara Supplies Company Limited, alipewa zabuni katika shirika hilo kwa kutumia taarifa za kughushi. Pia CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo haikuwasilisha katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), rejesho la kodi kiasi cha Sh4.854 milioni ilizolipwa na Tanesco.
Santa Clara
CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa Aprili 18, 2011, ilipewa Leseni ya Biashara, Mei 2011 na kwamba wakurugenzi na wanahisa wa kampuni ni mke na watoto wawili wa Mhando. Mke wa Mhando aliwahi kuwa mfanyakazi wa Tanesco, lakini aliacha kazi baada ya mumewe kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
CAG amebainisha kampuni hiyo iliingia mkataba na Tanesco na kupewa zabuni Namba PA/001/11/HQ/G/011 ya ugavi wa vifaa vya ofisi, vifaa vya matumizi ya kompyuta na mashine za kudurusu, kwa mwaka 2011 hadi 2012, mkataba ulianza Desemba 20, 2011.

CHANZO: Gazeti Mwananchi

Mashambulizi ya kushtua yatokea Somalia



Takriban watu kumi na tisa wameuawa katika shambulio la bomu na risasi mjini Mogadishu Somalia.
Wengine kumi na sita wakiwemo washambuluaji tisa pia wanasemekana kuuawa baada ya mtu aliyekuwa amejihami kuvamia majengo ya mahakama na kuanza kushambulia watu kiholela.
Baadaye bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari lilipuka kando ya barabara inayoelekea katika uwanja wa ndege ambako wafanyakazi wawili wa misaada wa Uturuki walikuwepo
Kundi la wapiganaji la al-Shabab linasema ndilo limefanya shambulio hilo.
Al-Shabab, ambalo lina uhusiano na al-Qaeda, limelaumiwa kwa mashambulio kadhaa mjini Mogadishu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Lakini wadadisi wanasema kuwa mashambulizi yaliyotokea hapo jana ndio mabaya zaidi kushuhudiwa tangu wapiganaji wa Al Shabaab kufukuzwa Mogadishu mwaka 2011.
Sasa shambulio hilo limesababisha hali ya hofu miongioni mwa wakaazi wa Mogadishu.
Sio eti ni mashambulizi makubwa kuwahi kushuhudiwa Mogadishu , bali yametokea huku wakaazi wa Mogadishu ukianza kuwa mji wenye utulivu.
Mashambulizi hayo bila shaka yatakuwa changamoto kubwa kwa serikali katika mji mkuu. Polisi wamepelekwa katika miji mikubwa ili kutoa ulinzi kwa majengo ya serikali.
Lakini serikali katika siku za nyuma ilikubali kuwa inaweza tu kufanya kadri ya uwezo wake kujaribu kuzuia washambuliaji wa kujitoa mhanga.
Vifo vya wafanyakazi wa misaada kutoka Uturuki, pia vitazua wasiwasi miongoni mwa idadi inayoongozeka ya mashirika ya misaada inayofanya kazi Somalia.

Chanzo: BBC