Saturday, June 30, 2012

Morsi aapishwa mjini Cairo

Kiongozi wa mwanzo wa Misri aliyechaguliwa kwenye uchaguzi huru, Mohammed Morsi, amekuwa rais mpya baada ya kuapishwa mbele ya mahakama ya katiba mjini Cairo.
Bwana Morsi kutoka chama cha Muslim Brotherhood anakuwa rais wa mwanzo wa chama cha Kiislamu, na wa kwanza ambaye hatoki katika jeshi.
Chama chake kilikuwa kimepigwa marufuku wakati wa utawala wa Rais Mubarak.
Ameahidi kuwalinda watu wa Misri, na kuheshimu katiba na sheria.
Jaji mmoja kwenye sherehe hiyo ya kuapishwa kwa rais, alisema leo ni siku kubwa kwa Misri, ukurasa mpya wa heshima na mafanikio.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo anasema watu walishangaa kuona ulinzi ni mchache katika eneo la mahakama ya katiba, kuonesha kuwa Bwana Morsi anataka kuwa mtu wa watu.
Hapo jana, Bwana Morsi alikula kiapo cha alama tu, mbele ya mamia ya wafuasi wake katika medani ya Tahrir, mjini Cairo - chimbuko la mapinduzi yaliyomuondoa Rais Mubarak.
Lakini mwandishi wetu anasema, haijulikani jeshi litampa rais mpya kiwango gani cha madaraka.

Mkutano wa kimataifa juu ya Syria waanza

Mkutano wa kimataifa unaoazimia kumaliza mzozo wa Syria unafanywa mjini Geneva, huku bado kukiwa na tofauti baina ya Urusi na mataifa ya magharibi, kuhusu jee rais wa Syria anafaa kubaki au la.

Urusi, ambayo imekuwa ikiisaidia serikali ya Rais Assad kwa hali na mali, imepinga madai kwamba Rais Assad anafaa kuondolewa madarakani.
Lakini baada ya kuzungumza na Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, alishikilia kwamba kuna matumaini makubwa ya kupata makubaliano.
Bi Clinton kwa uapnde wake alisema bado kuna tofauti na matatizo baina yao.

Iringa Ya Ibamiza Pemba 3-0,COPA COCA-COLA

Iringa imezinduka kwenye michuano ya Copa Coca-Cola baada ya leo asubuhi (Juni 30 mwaka huu) kuifunga Kaskazini Pemba mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani.
Hadi dakika 45 za kwanza za mechi hiyo ya kundi B zinamalizika matokeo yalikuwa suluhu. Mabao ya washindi yalifungwa na Goodluck Jonas dakika ya 51, Musa Maginga dakika ya 67 na Ramadhan Kiwelu dakika ya 70.

Iringa ilipoteza mechi zote mbili za kwanza dhidi ya Mwanza na Mjini Magharibi. Mbele ya Mwanza ilifungwa 3-1 wakati kwa Mjini Magharibi ikachezea kichapo cha mabao 3-0.

Katika mechi nyingine zilizochezwa asubuhi, Tabora iliichapa Shinyanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Mabao hayo yalifungwa na Said Juma na Ramadhan Mbalamwezi katika kila kipindi.

Nayo Ilala imepata pointi yake ya kwanza katika michuano hiyo baada ya kutoka suluhu na Kusini Pemba katika mechi ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam. Mjini Kibaha mkoani Pwani kwenye Uwanja wa Tamco, Dodoma iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtwara.


WINFRIDA DOMINIC NDIYE MISS UNIVERSE TANZANIA 2012


YANGA YATANGAZA KOCHA MPYA

"Tumeshamalizana naye na atatua Jumapili, tutawatangazia mashabiki utaratibu wa mapokezi wakati wa mechi yetu na Express (ya leo Jumamosi) lakini kimsingi kila kitu kimekamilika na wiki ijayo ataanza kazi baada ya kusaini mkataba.

Dogo Janja "Siko Tayari Kurudi Tip Top"

Si unafahamu kwamba Dogo Janja alirudi kwao Arusha baada ya kujiondoa TIP TOP lakini akarudishwa Dar na kundi la WATANASHATI ambalo ndio yuko nalo sasa hivi?

Sasa stori ni kwamba Baada ya meneja wake wa sasa wa WATANASHATI kusema kwamba yuko tayari kumuachia Dogo Janja kuchukuliwa na mtu yeyote ambae ataweza kumuendeleza vizuri kisanii na kimasomo hata TIP TOP wenyewe kama wakijirekebisha, Janja ameamua kutoa maneno matano kuhusu kurudi Tip Top kama wakijitokeza kwa hiyo ofa.


Amesema “Mimi kama mimi siko tayari”


Meneja Ostaz Juma alitangaza hiyo ofa juzi exclusive kwenye AMPLIFAYA ya CLOUDS FM na kusema yeyote atakae taka kumchukua Janja mikononi mwake itabidi amlipe gharama alizotumia, kauli ambayo iliwashtua wengi japo mpaka sasa Janja yuko mikononi mwa WATANASHATI.

Friday, June 29, 2012

Madaktari bingwa nao wagoma


TUKIO la kutekwa nyara, kupigwa na kujeruhiwa vibaya, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka, limechochea kasi ya mgomo baada ya madaktari bingwa kutangaza kujitosa rasmi kwenye mgogoro huo.Awali madaktari hao hawakushiriki mgomo huo, lakini jana walieleza kwa nyakati tofauti kuwa, wameamua kuungana na wenzao kutokana na unyama aliofanyiwa kiongozi wao akiwa katika harakati za kutetea na kupigania haki zao.

Madaktari hao wa hospitali za Muhimbili, Moi, KCMC, Mbeya, Bugando na Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuwa wameingia kwenye mgomo huo kushinikiza pamoja na mambo mengine, Serikali kutoa tamko kuhusu utata wa tukio hilo.

Tukio hilo la aina yake kutokea nchini, limeathiri upatikanaji wa huduma zote za matibabu katika hospitali hizo, huku madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Moi, wakielekeza nguvu zao kunusuru maisha ya mwenzao aliyeumizwa.

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mgomo huo utaendelea hadi hapo Serikali itakapotekeleza madai yao.

"Tunaitaka Serikali kuacha vitisho kwa madaktari nchini, tunaitaka itambue kwamba mgogoro huu hauwezi kumalizwa kwa njia yoyote vikiwemo vitisho bali ni kwa kukaa meza ya majadiliano na kukubaliana na madaktari," alisema Dk Chitega na kuongeza:

"Ninawashukuru madaktari wote nchi nzima, wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya kwa ujumla wao kwa kusitisha huduma baada ya kupigwa mwenzetu. Tunaomba mshikamano huu uendelee," alisema Dk Chitega.

Gazeti hili lilishuhudia wagonjwa wakiwa wamekaa katika makundi bila kujua la kufanya, huku wengine wakiamua kuondoka na kwenda hospitali binafsi.

Waliliambia Mwananchi kwamba kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na kuungana na madaktari hao kuitaka Serikali kutatua mgogoro huo haraka.

Wagonjwa waliofika katika eneo hili pia walielezwa bayana na maofisa wa Moi kwamba huduma zimesitishwa  kutokana na madaktari kugoma.

Ocean Road

Madaktari bingwa katika Taasisi ya Ocean Road nao waligoma kutoa huduma hatua iliyozua taharuki kwa wagonjwa waliofika kwa ajili ya matibabu.

Gazeti hili lilishuhudia ofisi za madaktari hao zikiwa zimefungwa na hata zile ambazo zilikuwa wazi, madaktari hawakuwapo.

Mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Dachi, alisema kuwa, wagonjwa wengi wamekuwa wakiandikishwa mapokezi, lakini wanachukua muda mrefu kumuona daktari.


Mgomo huo pia umeendelea katika Hospitali ya Amana wilayani Ilala huku uongozi wa hospitali hiyo ambao uligoma kuzungumza na vyombo vya habari, ukihaha kunusuru hali hiyo.

Katika Hospitali za Temeke na Mwananyamala huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida.

Mbeya

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ,madaktari bingwa ambao awali hawakugoma jana waliingia kwenye mgomo na kusababisha wagonjwa katika hospitali hiyo hususan kitengo cha wazazi, kusota bila matibabu.

Habari kutoka katika hospitali hiyo zilieleza kuwa hivi sasa madaktari bingwa wanatoa huduma kwa kujuana.

Mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kitendo alichofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya yao kimewakatisha tamaa.

Alisema kuwa, hali hiyo sasa imehamia hadi katika Kituo cha Wazazi cha Meta na kufafanua kuwa hali ni mbaya, tayari wajawazito wametakiwa kuhamia katika Hospitali ya Mkoa ambayo imefurika wagonjwa.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo ya Rufaa, Dk Eliuter Samky hakuweza kuzungumzia tukio hilo jana kutokana na kile kilichoelezwa na katibu wake muhtasi kwamba ana kazi nyingi.

Mwanza
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) mkoani Mwanza nao wamegoma, huku kiongozi wa Kamati Ndogo ya hospitali hiyo inayoshughulikia migomo, akikataa kuzungumzia hali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu baada ya kutoonekana katika maeneo ya hospitali, mmoja wa viongozi wa Kamati hiyo, Dk Geogre Adrian, alisema kwa sasa hawezi kulitolea ufafanuzi suala hilo na kwamba kufanya hivyo, ni kwenda kinyume na maagizo aliyopewa na Kamati Kuu.


Akizungumzia huduma katika hospitali hiyo alisema kuwa hajui lolote kwa kuwa hawajagusa maeneo ya kazi kwani  wapo kwenye mgomo.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia huduma katika hospitali yake, hakupatikana.

Watimuliwa
Jana Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Charles Majinge alitoa tangazo la kuwataka madaktari waliopo mafunzoni ‘Interns’ katika hospitali hiyo kurejea kazini na kama watakiuka agizo hilo, watakuwa wamejifukuzisha wenyewe.


Manyara
Mkoani Manyara, madaktari kumi katika Hospitali ya Haydom Wilaya ya Mbulu wamegoma tangu juzi.Idadi ya wagonjwa katika hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), inaongezeka siku hadi siku.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotaka kutajwa majina yao, madaktari hao ambao wanafanya mafunzo ya vitendo katika hospitali hiyo, wamesema kuwa hawatatibu wagonjwa mpaka madai yao yatekelezwe.


Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Anatory Choya, alithibitisha kutokea kwa mgomo huo na kufafanua kwamba wanaendelea kufanya mazungumzo ili kupata ufumbuzi.

Choya alisema kuwa madaktari wanaoendelea na kazi, wameelemewa  kutokana na wagonjwa kuwa wengi.

Alisema kati ya madaktari 11 wanaosoma kwa vitendo hospitalini hapo, mmoja tu anayesomeshwa na hospitali hiyo, ndiye hajagoma.

KCMC
 Hali katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro imezidi kuwa tete na kuwafanya ndugu kuwahamishia wagonjwa wao katika hospitali binafsi.

Mwananchi lilitembelea wodi za hospitali hiyo na kukuta vitanda vikiwa wazi.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya madaktari ambao wapo kwenye mgomo kwa sharti la kutotajwa majina, walisema hawako tayari kurudi kazini kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Dodoma
 Wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma jana walijikuta wakipata taabu baada ya madaktari wa hospitali hiyo kusitisha huduma kwa takriban saa sita kuanzia asubuhi.

Muda wa mchana utoaji huduma katika hospitali hiyo uliendelea ingawa kwa  kusuasua.

Tofauti na siku zote, jana chumba cha daktari kilichokuwa wazi ni kimoja tu hali iliyosababisha msongamano mkubwa.


Arusha

Mjini Arusha, madaktari wameendelea na mgomo katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na kusababisha kudorora huduma huku wagonjwa kadhaa wakiondolewa hospitalini hapo.

Mgomo huo, ulianza saa 1 asubuhi hadi saa 6:00 mchana, ambapo madaktari na wauguzi,waligoma kutoa huduma wakitaka kujua hatima ya Dk Ulimboka. Walitaka pia kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo na waandishi wa habari, kuhusu mgogoro wao.

Askari anyimwa huduma

Askari wa Usalama Barabarani ambaye jina lake halikufahamika mara moja ambaye alipata ajali jana, alijikuta akishindwa kuhudumiwa katika hospitali ya Mount Meru na kuondolewa kutokana na mgomo huo.

Askari huyo, aliyevaa sare, alifikishwa hospitalini hapo saa 5:00 asubuhi akiwa kwenye teksi, lakini wauguzi waliokuwa zamu walishauri apelekwe sehemu nyingine.

Hata hivyo, uongozi wa hospitali ya mkoa, ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Omar Chande, jana ulifanya kazi ya ziada ya kuwabembeleza madaktari hao, kurejea kazini, kusubiri uamuzi wa Serikali.



Mgomo, Dk Ulimboka
vyateka Bunge

Mgomo wa madaktari na kutekwa kisha kupigwa Dk Ulimboka jana vilitawala mjadala wa Bunge hadi pale Spika Anne Makinda alipotoa mwongozo kwamba suala hilo lisijadiliwe kwani liko mahakamani.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilazimika kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa juzi pale alipokuwa akizungumzia mgomo wa madaktari na kuhitimisha kwamba Serikali ilikuwa inajiandaa kutoa kauli na msimamo wake hivyo “liwalo na liwe’.

Pinda alilazimika kutoa maelezo kutokana na swali aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kufahamu maana ya kauli ya Waziri Mkuu ambayo aliita kuwa ni nzito na iliyozua mjadala mkali nchini.

Kadhalika, Mbowe alitaka kufahamu hatua ambazo Serikali imechukua kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma za tiba kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba madaktari katika hospitali kadhaa walikuwa wakiendelea na mgomo.


Kadhalika Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alimuuliza Pinda kwamba haoni kwamba ni busara kujiuzulu wadhifa wake kutokana na ahadi yake kwamba mgomo wa madaktari usingetokea, lakini ahadi hiyo imeshindwa kutekelezeka.

Akimjibu Mbowe, Pinda alikiri kutoa kauli hiyo ndani ya Bunge juzi na kusema alifanya hivyo akiamini kuwa jambo hilo lilikuwa mahakamani na akasema asingeweza kusema jambo lolote kwa kuwa hana tabia ya kuwa na utovu wa nidhamu wa kuingilia mambo ya mahakamani.

Hata hivyo, alijitetea kuwa kabla ya kutoa kauli hiyo bungeni juzi, hakuwa na taarifa kuhusu tukio la kupigwa kwa Ulimboka na akasema kuwa, kauli yake haihusiani kabisa na Serikali kuhusika katika jambo hilo kwa namna yoyote ile.

Waziri Mkuu alisema tayari amekwishaagiza vyombo husika kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu ya haraka ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki mara moja.

“Kwanza namtakia afya njema ndugu Ulimboka, na mimi nataka Watanzania waamini kuwa tulikuwa katika mazungumzo mazuri na madaktari chini yake Ulimboka hivyo tukio hilo ambalo limetokea katika mazingira magumu limetushtua kweli, kama ni Serikali basi ingekuwa ni Serikali ya ajabu kweli,’’alisema Pinda.

Kuhusu namna ya kusaidia Watanzania wasiathirike na mgomo huo, alisema tayari Serikali imeshaagiza madaktari kutoka wizarani kutumika na kuwaomba waliostaafu kutoa huduma katika kipindi hicho kigumu.

Mkakati mwingine ni pamoja na kutumia hospitali za Jeshi ikiwamo Lugalo waanze kutoa huduma hizo wakati Serikali inaendelea kuzungumza kwa utaratibu na madaktari.

Lissu aliuliza swali la nyongeza kumtaka Pinda kuachia ngazi hali iliyosababisha mvutano kwani Waziri Mkuu alikosoa uulizaji wa swali hilo kuwa halikustahili.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala la madaktari akitaka taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ambayo ilifanyia kazi suala la mgomo wa madaktari ijadiliwe bungeni.

Hata hivyo, Spika Makinda alisema ripoti hiyo haiwezi kujadiliwa kwani tayari Serikali ilishakabidhiwa kwa ajili ya kuifanyia kazi na kwamba mapendekezo ya Bunge kupitia ripoti hiyo yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa.


Habari hii imeandaliwa na Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma, Godfrey Kahango,Mbeya, Joseph Lyimo,Mbulu, Sheilla Sezzy,Mwanza, Rehema Matowo, Moshi, Masoud Masasi,Dodoma, Fidelis Butahe, Geofrey Nyang'oro Dar, Mussa Juma, Arusha, Bakari Kiango na Victoria Mhagama
     

Daktari: Hali ya Ulimboka mbaya

ASEMA FIGO ZAKE ZIMESHINDWA KAZI, ZATAKIWA DOLA 40,000 KUMPELEKA INDIA
Geofrey Nyang’oro na James Magai
AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka imebadilika na kuwa mbaya, baada ya figo zake kushindwa kufanya kazi ya kuchuja sumu ya mwili na kusababisha apatiwe huduma ya kusafisha damu yake.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na kiongozi wa jopo la madaktari wanaoendelea kumtibu, Profesa Joseph Kahamba, zilieleza kuwa hali ya Dk Ulimboka ilibadilika na kuwa mbaya na hivyo kuwapo mikakati wa madaktari wenzake kukusanya fedha ili kumpeleka nje ya nchi.

Dk Ulimboka ambaye amelazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI), alipatiwa huduma hiyo jana asubuhi kwa kutumia mashine maalumu, iliyoko katika Kitengo cha Watoto cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Daktari huyo ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima kutokana na Serikali kushindwa kutimiza madai yao mbalimbali, amelazwa kutokana na majereha aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa kucha, meno mawili na kutupwa katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia Jumatano.

Tangu alazwe MOI baada ya kuokotwa na wasamalia wema, katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dares Salaam, hali ya afya ya Dk Ulimboka imekuwa tete na jana ilizidi kuwa mbaya.

Kauli ya Dk Kahamba

Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Kahamba alisema kutokana na tatizo hilo, mgonjwa huyo jana alilazimika kusafishwa damu.

Alieleza hayo alipotakiwa kuthibitisha taarifa zilizolifikia gazeti hili kuwa afya ya Dk Ulimboka haikuwa nzuri na madaktari wanachangishana fedha kumpeleka kwenye matatibu ya kusafishwa damu katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam au nje ya nchi.

"Taarifa hizo zina ukweli, lakini siyo jambo rahisi kiasi hicho kwamba anatakiwa kusafishwa damu. Kama ni damu amesafishwa leo (jana) asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili," alisema Profesa Kahamba na kuendelea:

"Suala lake ni complicated (tata) zaidi, lakini ili watu waelewe, siyo mbaya mkisema figo zimefeli(zimeshindwa kufanya kazi)."

Alipotakiwa kueleza sababu ya tatizo hilo, Profesa Kahamba alisema, "Siwezi kueleza kwa undani ila haya maumivu ya kupigwa na kuteswa yanachangia kwa kiasi kikubwa."

Alipotakiwa kueleza yeye anaonaje hali ya sasa ya Dk Ulimboka, Profesa Kahamba alisema: “Ni uongo tukisema anaendelea vizuri."

Aliendelea, "Unajua alipofikishwa hapa Muhimbili juzi (Jumatano) afya yake ilikuwa mbaya, na jana (Alhamisi) alionekana kuendelea vizuri, lakini jana hiyohiyo, hali yake ilianza kubadilika na vipimo vilionyesha kuwa ana complications (matatizo) za figo.

"Sasa figo ni kitu sensitive (muhimu) sana, anahitaji uangalizi wa karibu na kimsingi hatuwezi kusema kwamba anaendelea vizuri. Ni vyema tukisema tu afya yake ni mbaya," alieleza.

Taarifa za awali kutoka kwenye chanzo chetu hospitalini hapo, zilieleza kuwa Dk Ulimboka ambaye alipata tatizo linalojulikana kama “Acute renal failure”, alifanyiwa tiba inayojulikana kama Dialysis, ambayo ni kitendo kutumia mashine maalumu kufanya kazi ya kuchuja sumu ya mwili kwenda kwenye mkojo, baada ya figo ambazo hufanya kazi hiyo kushindwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Dialysis inaweza kumsadia mgonjwa ambaye figo zake zimeshindwa kufanya kazi, kuishi kama kawaida, lakini kwa Dk Ulimboka haikutoa matokeo mazuri.

Michango ya madaktari

Jana ulifanyika Mkutano wa Madaktari Bingwa wa MNH, Chuo Kikuu Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ocean Road (ORCI) na kuazimia kukusanya Dola za Marekani 40,000 (Sh64,000,000) ili Dk Ulimboka asafirishwe kwenda India kwa matibabu zaidi.

Taarifa za maazimio hayo zilitangazwa kwa waandishi wa habari na Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitega, kuwa afya ya Dk Ulimboka haikuwa nzuri hivyo zikipatikana fedha hizo angepelekwa nje ya nchi.

Dk Chitega aliwataka wanataaluma hao na wananchi kwa ujumla kuchangia safari hiyo ili kuokoa maisha ya daktari huyo, huku akitaja namba za mawakala wa simu za Vodacom na Tigo, ambazo zitatumika kukusanya michango hiyo.

Habari zilizopatikana baadaye wakati tunakwenda mitamboni zilieleza kuwa, Dk Ulimboka alitarajiwa kusafirishwa kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.


TANNA MOI watoa tamko
Katika hatua nyingine, Chama cha Wauguzi (Tanna), Tawi la MOI kilitoa tamko la kulaani kitendo cha kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka na kutaka uchunguzi wa kina na haraka ufanyike ili kubaini watu waliohusika.

Mwenyekiti wa Tanna, Tawi la Moi, Prisca Tarimo alisema katika tamko hilo kuwa, kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na kisicho cha kiutu.

Katika tamko hilo, Tanna imeomba Serikali kutafuta suluhu ya mgomo huo haraka kwa kuwa unaathiri maisha ya watu na kuwaongezea mzigo wa kiutendaji wauguzi.

Mgomo wa madakati unaingia siku ya saba leo, huku suluhu ya kuaminika ya kutatua tatizo hilo, ikiwa bado haijapatikana.

Polisi wakanusha
Katika hatua nyingine, James Magai anaripoti kuwa, Jeshi la Polisi limekanusha kumteka na kumjeruhi Dk Ulimboka, huku likipinga pia taarifa za daktari huyo kumtambua mmoja wa askari walio katika jopo la uchunguzi wa tukilo hilo alipokwenda kumtembelea hospitalini.

Pia jeshi hilo limetoa wito kwa madaktari hao walioko katika mgomo kuwa na busara na kutii amri ya Mahakama, ya kuwataka wasitishe mgomo wao.

Pia limeonya kuwa ikiwa wataendelea kukaidi na kupuuza amri ya hiyo ya mahakama, linao wajibu wa kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha mahakamani, ili wajibu mashtaka hayo.

Msimamo huo ulitolewa jana na Kamishna wa Oparesheni Maalumu, Kamishna wa Polisi (CP), Paul Chagonja wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano alioitisha kuzungumzia matokeo ya operesheni ya jeshi hilo ya majuma matatu katika kuzuia uhalifu nchini.

Alisema madai hayo ni uvumi ambao unalenga kulifanya jeshi hilo lisiaminike na kufifisha juhudi zake za kuwasaka waliohusika na unyama huo. 

( CHANZO:GAZETI MWANANCHI)

Dawa mpya kwa wagonjwa wa Ukimwi

Huenda wagonjwa wa Ukimwi wakanufaika na dawa mpya ambayo itawawezesha kutumia tembe moja kwa siku. Hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya nchini Marekani.
Jarida la Afya Lancet limesema tembe hiyo inajumlisha dawa zote nne zinazokabiliana na makali ya ukimwi na kwamba ni salama.Utafiti unasema hii itawarahisishia wagonjwa katika kuhakikisha wanafuata maagizo ya madaktari wao.
Ukimwi hauna tiba lakini watafiti wameweza kutoa dawa za kukabiliana na maradhi nyemela.
Watafiti pamoja na kampuni za dawa wamechanganya dawa nne na kutengeneza tembe moja ili kurahisisha utumizi wa dawa hiyo miongoni mwa wagonjwa.
Tembe inayofanyiwa majaribio na ambayo imechanganywa dawa nne inauwezo wa kudhibiti virusi vya HIV kuongezeka mwilini.
Paul Sax mtafiti mkuum katika Hospitali ya Wanawake ya Brigham huko Boston,Massachussetts ambaye pia ni mwanazuo wa ziada wa taasisi ya afya ya Harvard ameelezea umuhimu wa tembe hii kwa kuimarisha afya ya wagonjwa.
Dk. Sax ameongoza utafiti huu ambapo pia wamefanyia majaribio tembe hii kwa wagonjwa 700 na kusema inafanya kazi, japo kulitokea matatizo ya figo miongoni mwa waliotumia.
Licha ya mafanikio ya sasa watafiti wanasema raia wengi hawafahamu hali zao ambapo wameendelea kuishi na maambukizi bila kujua.

Wageni watekwa wakiwa kambini Kenya

Polisi nchini Kenya wamesema kuwa wafanyikazi sita wa shirika la kutoa misaada kwa wakimbizi wametekwa nyara katika kambi ya wakimbizi ya Ifo ilioko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
kambi hiyo inatoa hifadhi wakimbizi nusu milioni
Waliotekwa ni wafanyikazi wa shirika la Norwegian Refugee Council, ambalo linatoa huduma kwa wakimbizi kutoka Somalia wanaoishi kwenye kambi hiyo.
Msemaji wa Shirika hilo, amedhibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa katibu mkuu Elizabeth Rasmussen alikuwemo kwenye msafara uliovamiwa lakini amenusurika.
Hata hivyo shirika hilo halijatoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo na watu waliotekwa.
Mkuu wa wilaya ya Lagdera ambako kambi hiyo ipo Robert Kimanthi amesema waliotekwa ni raia wa Canada, Norway, Mfilipino, Mpakistani na Wakenya wawili. Wote ni wanaume.
Kulingana na polisi watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki walishambulia msafara wa magari katika kambi hiyo ambayo inatoa makaazi kwa zaidi ya wakimbizi nusu milioni kutoka Somalia. Mtu mmoja aliuawa kwenye tukio hilo.
Polisi wanashuku kuwa wapiganaji wa kiisalamu wa Al shaabab walihusika na shambulio hilo.
Visa vya mashambulio ya kigaidi vimeongezeka katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya, baada ya wanajeshi wake kuingia nchini Somalia mwaka jana kupambana na wanamgambo wa al shabaab.
Katika miezi ya hivi karibuni, wafanyakazi kadhaa wa mashirika ya kutoa misaada wametekwa nyara katika kambi hiyo ya Daadab.
Wawili kati yao ni wanawake wawili raia wa uhispania ambao walitekwa nyara mwezi Oktoba mwaka uliopita.

NAMNA HII TUNAJENGA TAIFA GANI?


MISS REDD'S IRINGA ILIJAWA NA VITUKO, JAJI MKUU AZOMEWA

Huyu  ndie Naomi  James  ambaye  ametawazwa  usiku  huu kuwa  Miss Redd's mkoa  wa  Iringa na  kuzawadiwa  kitita cha  shilingi 500,000

HIVI HUYU MZEE YUPO?


INAKUWAJE IKIKUTOKEA HII?



USWAZI KUNA MAMBO


HALI YA HOSPITALI ZETU


DAKTARI ULIMBOKA ANAENDELEA VIZURI NA MATIBABU MUHIMBILI


KUMBE 'WABANA PUA' HUFANYA HIVI


Wednesday, June 27, 2012

ALICHOKIANDIKA ZITTO KABWE KUHUSU DR ULIMBOKA KUTEKWA NA KUPIGWA.





Hali ya Dk. Ulimboka si shwari sana

Hivi ndivyo Dk. Ulimboka alivyokutwa na kituo cha sheria na haki za binadamu baada ya kutolewa kituo cha polisi BUNJU. PICHA NA LHRC

GARI LA BIA LAPATA AJALI SUMBAWANGA...WANANCHI WALEWA CHAKARI


Kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi.....baada ya ajaali hiyo kutokea kijiji cha Mshani km 19 kutoka Laela-Sumbawanga ilikuwa kama sherehe kwa wengine kwani wanakijiji walivamia gari na wakaruhusiwa kunywa watakavyo ila hakuna kuondoka na chupa.....asubuhi watu walikuwa wamelewa chakari...Maisha bora kwa kila Mtanzania

MASANJA NAE ANA MAMBO

YUPO MKOANI IRINGA KIKAZI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Juni 27, 2012

POLISI MORO YAACHA 17, TZ PRISONS 11


Klabu tano za Ligi Kuu ya Tanzania zimewasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) majina ya wachezaji ambao zimewakatishia mikataba/mikataba yao kumalizika au kuwaacha kwa ajili ya usajili wa wachezaji msimu wa 2012/2013.


Kwa mujibu wa klabu hizo, Polisi Morogoro iliyopanda msimu huu imeacha wachezaji 17 wakati Tanzania Prisons ambayo pia imepata hadhi ya Ligi Msimu huu imeacha wachezaji 11. Azam imekatisha mikataba ya wachezaji watatu.


Wachezaji 12 wamemaliza mikataba yao katika klabu ya Kagera Sugar wakati wakati kwa upande wa Simba wachezaji waliomaliza mikataba ni wanne huku ikionesha nia ya kuwatoa kwa mkopo wengine wanne.


Uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 mwaka huu na utamalizika Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuanza wachezaji (kwa wasio wa Ligi Kuu) ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu.


Kwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu.


Wachezaji walioachwa Polisi Morogoro ni Abdul Ibadi, Ally Moshi, Benedict Kitangita, Hassan Kodo, Hussein Lutaweangu, Hussein Sheikh, Juma Maboga, Mafwimbo Lutty, Makungu Slim, Mbaraka Masenga, Method Andrew, Moses Mtitu, Ramadhan Kilumbanga, Ramadhan Toyoyo, Said Kawambwa, Salum Juma na Thobias John.


Tanzania Prisons imewaacha Adam Mtumwa, Dickson Oswald, Exavery Mapunda, Ismail Selemani, Lwitiko Joseph, Mbega Daffa, Mwamba Mkumbwa, Musa Kidodo, Rajab Ally, Richard Mwakalinga na Sweetbert Ajiro.


Wachezaji waliomaliza mikataba yao kwa mujibu wa Kagera Sugar ni Cassian Ponera, Hamis Msafiri, Hussein Swedi, Ibrahim Mamba, Martin Muganyizi, Mike Katende, Moses Musome, Msafiri Davo, Said Ahmed, Said Dilunga, Steven Mazanda na Yona Ndabila.


Azam imewasitishia mikataba wachezaji Tumba Swedi, Mau Bofu na Sino Augustino. Wachezaji waliomaliza mikataba Simba kwa mujibu wa klabu hiyo ni Ally Mustafa, Derick Walulya, Gervais Kago, Juma Jabu wakati Salum Kanoni mkataba wake unatarajia kumalizika Juni 30 mwaka huu.


Wachezaji ambao Simba inakusudia kuwatoa kwa mkopo ni Rajab Isihaka, Salum Machaku, Haruna Shamte na Shija Mkina.


DODOMA YAITAMBIA MBEYA COPA COCA-COLA 2012


Dodoma imeendeleza wimbi la ushindi kwenye michuano ya Copa Coca-Cola 2012 baada ya leo asubuhi (Juni 27 mwaka huu) kuifunga Mbeya mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tamco ulioko Kibaha mkoani Pwani.


Mabao ya Dodoma katika mechi hiyo ya kundi C yalifungwa na Japhet Lunyungu dakika ya 59 wakati Frank Kaji aliwahakikishia ushindi washindi dakika saba kabla ya filimbi ya mwisho baada ya kupachika bao la pili.


Nayo Mjini Magharibi iliifunga Iringa mabao 3-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa leo asubuhi kwenye Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani.


Mechi za asubuhi zilizokuwa zichezwe leo kati ya Arusha na Kusini Pemba kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers na Pwani na Tabora kwenye Uwanja wa Karume sasa zitachezwa kuanzia saa 8 mchana kutokana na kutokuwepo mawasiliano ya barabara asubuhi (Morogoro Road) kutoka mkoani Pwani kuingia Dar es Salaam.


Leo jioni kutakuwa na mechi kati ya Rukwa na Ruvuma (Tanganyika Packers), Mwanza na Tanga (Nyumbu), Kaskazini Unguja na Mara (Tamco) na Singida na Kagera (Karume).


Boniface Wambura


Ofisa Habari


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

'MWANAMKE WAKE MKOBA'


BAADHI YA MAGAZETI YA LEO J'TANO 27/6/2012