Askofu Ngalalekumtwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amempongeza Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kwa kuteuliwa kwake kuwa
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) akichukua nafasi ya Baba
Askofu Yuda Tadei Rwaich aliyemaliza muda wake.
“Nimefarijika sana na
uteuzi wako kushika wadhifa huo muhimu hasa kutokana na imani kubwa waliyonayo
Maaskofu kuhusiana na uwezo wako katika kukiongoza chombo hicho muhimu”, amesema
Rais Kikwete katika salamu zake.
“Ninatambua
na kuthamini mchango mkubwa ambao, kwa muda mrefu sasa, Kanisa Katoliki limekuwa
likiutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake hasa katika nyanja za huduma za
jamii.
Aidha uhusiano mzuri uliopo kati ya
Serikali ninayoiongoza na Kanisa Katoliki unaendelea kunitia moyo, hivyo
ninakuhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza na kuimarisha
uhusiano huu kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla”, amesema na
kusisitiza Rais Kikwete katika salamu zake za
pongezi.
Rais Kikwete amemtakia Baba Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa kila la heri na mafanikio makubwa katika kuliongoza
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Imetolewa na:Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.Dar es Salaam.
|
No comments:
Post a Comment