Monday, August 26, 2013

Mubarak afikishwa mahakamani



Aliyekuwa rais wa Misri, Hosni Mubarak, amefikishwa mahakamani, siku tatu baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani na kuwekwa katika kifungo cha nyumbani.
Mubarak amefunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji wakati wa mageuzi yaliyomuondoa madarakani mwaka wa 2011.
Rais huyo wa zamani alifika kizimbani akiwa na wanawe wawili wa kiume, waziri wa zamani wa usalama wa ndani na maafisa sita waandamizi wa ulinzi wakati wa utawala wake.
Awali, kesi nyingine inayomkabili generali mkuu wa vugu vugu la Muslim Brotherhood na manaibu wake wawili ilihairishwa.
Mahakama hiyo ilisikiliza kesi hiyo kwa muda mfupi na kuchukua uamuzi huo kwa sababu Mohammed Badie, Khairat al-Shater na Rashad Bayoumi hawakuwa mahakamani kwa sababu za kiusalama.
Watatu hao waliamriwa kufika mahakamani tarehe ishirini na tisa mwezi huu wakati kesi yao itakaposikilizwa.
Viongozi wa chama cha Muslim Brotherhood wanakabiliwa na mashitaka ya kuchochea mauji ya waandamanji waliovamia makao makuu ya vugu vugu la Kiisalamu mjini Cairo tarehe thelathini mwezi Juni mwaka huu, wakati mamilioni ya raia wa nchi hiyo walipoandamana kutaka kujiuzulu kwa mrithi wa rais Hosni Mubarak, aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Morsi.
Lakini kiongozi huyo aliondolewa madarakani siku tatu baadaye na viongozi wa jeshi la nchi hiyo.
Morsi anazuiliwa na utawala wa kijeshi huku viongozi wa mashitaka wakiendelea na uchunguzi kubainisha jinsi alivyotoroka kutoka kizuizini wakati wa mageuzi yaliyomuondoa rais Mubarak madarakani na madai ya kupanga njama na kundi la kigaidi la Kiislamu nchini Palestina la Hamas.
http://www.bbc.co.uk/swahili

Monday, August 12, 2013

Hotuba ya Mugabe baada ya uchaguzi



Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza tangu kushinda uchaguzi mkuu wa Zimbabwe zaidi ya wiki moja iliyopita.
Mugabe atahutubia umma wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa mjini Harare kuwakumbuka wale waliofariki wakipigania uhuru wa taifa hilo.
Chama pinzani cha MDC, chake waziri mkuu Morgan Tsvangirai, kitasusia sherehe hizo.
Chama hicho kimewasilisha malalamiko yake kuhusu uchaguzi mkuu ambao kinasema ulikumbwa na wizi wa kura kikitaka uchaguzi huo kurejelewa.
Bwana Mugabe alishinda 61% ya kura kwenye uchaguzi huo uliokamilika tarehe 31 mwezi Julai, huku mpinzani wake Morgan Tsvangirai akichukua nafasi ya pili kwa 35% ya kura zilizopigwa.
Chama cha Mugabe Zanu-PF kilishinda wingi wa viti vya bunge kikipata zaidi ya thuluthi mbili ikiwa ni viti 160 ya viti kati ya 210 vya bunge zima.
Sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa Zimbabwe, ni sherehe za kujivunia kwa wazimbabwe wakati ambapo nchi hiyo ilijipatia uhuru wake miaka ya sabini.
Hii leo Mugabe atatoa hotuba yake ya kwanza katika eneo la kumbukumbu la vita hivyo na ambako baadhi ya wapigania uhuru wamezikwa.
Hotuba za Mugabe zinasifika zaidi kwa siasa zake kali za kizalendo, na ambazo zaidi hulenga mkoloni wake wa zamani Uingereza na pia anatarajiwa kujipiga kifua kufuatia ushindi wake mkubwa katika uchaguzi mkuu uliopita mwezi jana.
Chama cha MDC kinasusia sherehe hizo katika kile kinachosema ilikuwa wizi mkubwa wa kura uliofanywa na chama cha Zanu-PF, kwa hivyo sherehe hii bila shaka itazongwa na siasa.
Mugabe bado hajaapishwa kwa muhula wake wa saba akitawala Zimbabwe, kwa sababu ya kesi ya MDC mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
MDC kilisema kina ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa wizi wa kura ulitokea na kwamba kulikuwa na visa vingine vilivyohujumu matokeo ya uchaguzi huo ikiwemo, rushwa , dhuluma na kuvurugwa kwa daftari la wapiga kura.
http://www.bbc.co.uk/swahili

Sunday, August 11, 2013

Sheikh Ponda alindwa hospitali Dar


Sheikh Ponda
Jumuiya ya Taasisi za kidini za Kiislamu nchini Tanzania imeitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini na kuwachukulia hatua watu waliompiga risasi Sheikh Ponda Issa Ponda Jumamosi mjini Morogoro, Mashariki mwa nchi hiyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhajj Mussa Kundecha, amewaambia waandishi wa habari mjini humo kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya Tanzania.Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Dar es Salaam, Baruan Muhuza, sheikh huyo ambaye amekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na serikali ya nchi hiyo alipigwa risasi baada ya kutokea vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr.
Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini humo Advera Senso ameiambia BBC mjini Dar es Salaam kuwa jeshi lake kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.
Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe; hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini.
Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.

Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.

http://www.bbc.co.uk/swahili

Saturday, August 10, 2013

Wizi ulitokea wakati moto unawaka

Sehemu ya uwanja wa ndege wa Nairobi iliyoteketea
Askari polisi saba wanahojiwa na wachunguzi nchini Kenya, wakishukiwa kuhusika na uporaji wakati wa moto ambao uliteketeza eneo la mapokezi la uwanja wa kimataifa mjini Nairobi mwanzo wa juma. 

Askari hao, akiwemo inspector, wanashutumiwa kuiba pesa na ulevi.

Wafanyakazi wa uwanja wa ndege, uhamiaji na madereva wa taxi ni kati ya wale wanaohojiwa, baada ya kamera za usalama kuonesha watu wakiiba vitu madukani.

Wakuu piya wanawatafuta watu wane waliokuwa wakisubiri kufukuzwa nchini kabla ya moto huo kutokea.

Watu hao wametoweka.
Ijumaa Rais Uhuru Kenyatta alisema moto huo haukutokana na kitendo cha kigaidi.

http://www.bbc.co.uk/swahili/

Mtambo Dawa za Kulevya Waingizwa Nchini




WAKATI matukio ya baadhi ya vigogo na wasanii maarufu wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulenya hayajapoa, imebainika kuwa mtambo maalumu wa kuchanganya na kuziongezea thamani dawa hizo upo hapa nchini.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa mtambo huo ambao awali ulikuwa unapatikana Mombasa, Kenya, pekee, unatumika kuchanganya dawa za kulevya na kemikali nyingine ambapo nusu kilo ya heroine huongezwa hadi kufikia kilo mbili.
Uchunguzi unaonyesha kuwa kuwa mtambo huo ulioingizwa mwaka huu na kigogo mmoja wa dawa hizo, upo katika nyumba moja iliyopo eneo la Mbezi Beach. Mmoja wa watumiaji wa dawa hizo ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema mtambo huo umerahisisha upatikanaji wa heroine nchini maarufu ‘white sugar’ kama inavyojulikana mitaani.
“Zamani ‘white sugar’ ikitoka shamba (nchi inakotengenezwa yaani Pakistan na nchi nyingine) ilikuwa inapelekwa Mombasa, Kenya, ambako kuna mtambo wa kuchanganya na dawa nyingine ili iongezeke wingi wake, lakini kazi hiyo inafanyika hapa hapa nchini kwa sasa,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa mtambo huo hapa nchini, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema kuwa kuna taarifa alizonazo ambazo bado anazifanyia kazi.
“Hata kama nikiwa nazo nazifanyia kazi, za kwangu mimi nazifanyia kazi na hata za kwako nazifanyia kazi,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa akizungumza katika kipindi cha Malumbano ya Hoja kilichorushwa na Televisheni ya ITV juzi, alisema kuwa katika siku za hivi karibuni wafanyabiashara wa heroine wamekuwa wakiingiza nchini malighafi za dawa hizo, tofauti na awali ambapo walikuwa wakiingiza dawa hizo zikiwa tayari kwa matumizi.
Akitoa mfano alisema kuna raia wa kigeni alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akiwa na malighafi hizo zilizokuwa zikifanana na sukari na kwamba Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mkemia Mkuu wa Serikali, ndiyo waliobaini kuwa haikuwa sukari kama ilivyodhaniwa.
Alisema kutokana na uhaba wa dawa hizo bei ya kete imepanda ambapo hivi sasa hakuna kete ya gramu 0.11 inayouzwa chini ya Sh 3,000. Hii ni mara ya pili kubainika kuwepo kwa mtambo wa kutengenezea dawa za kulevya nchini. Miaka ya hivi karibuni jeshi la polisi lilikamata mtambo wa kutengenezea dawa za kulevya katika nyumba moja iliyopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya kuwepo mtambo huo kuna nyumba tano katika eneo la Tandika jijini Dar es Salaam karibu na soko, ambazo zinatumika kuuza dawa za kulevya huku baadhi ya polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, wakiwalinda wauzaji wake kwa kuwapa taarifa ya mipango inayopangwa na jeshi la kuwatia mbaroni.
Alisema kuna wakati askari huonekana wakirandaranda katika mitaa hiyo, kitu kinachowafanya wakazi wa maeneo hayo kuamini kuwa wamefika kukamata, lakini badala yake huishia kuingia katika nyumba hizo kuchukua hongo na kutoka.
“Hata askari wenyewe wakija kukagua hubaki wakishangaa na kushindwa kuamini kama kweli nyumba waliyoambiwa inauza unga ndiyo hiyo waliyoikagua. Ndiyo ‘madili’ hayo watu wanavyoishi mjini hapa,” alisema. Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Temeke, Engelbert Kiondo alisema hawezi kusema ndiyo au hapana kwa kuwa jambo hilo linahusisha vitendo vya rushwa.
“Kuhusu askari kuwalinda wahalifu siwezi kusema ndiyo au hapana kwa sababu hili ni suala la rushwa,” alisema Kiondo na kuongeza kuwa: “Lakini kuhusu kuwakamata vijana wanaojihusisha na dawa za kulevya hao tunawakamata kila siku, wengi wameshafikishwa mahakamani kesi zao zipo katika hatua tofauti.”
Kwa upande wake Nzowa, alisema kwamba Jumatano wiki hii walifanikiwa kuwakamata watu watatu wakijihusisha na dawa hizo, akiwamo mwanafunzi wa kike na kwamba wote walifikishwa mahakamani.
Taarifa zaidi ziliendelea kueleza kuwa dawa aina ya heroin au ‘white sugar’ ndiyo inayopatikana kwa wingi nchini huku ikifuatiwa na ‘cleck’ inayojulikana mitaani kama ‘pele’ kwa kuwa inatoka nchini Brazil.
“Bei ya unga hutegemea aina na kiwango mteja anachokihitaji kwani kipo kipimo cha Sh 1,000 na Sh 2,000 huku kipimo maarufu kama pointi kikiuzwa kati ya Sh3,000 na Sh3,500. Lakini pele huuzwa bei kubwa zaidi, kwani ukubwa wa punje ya mtama tunanunua kwa Sh10, 000,” alifafanua.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz

WAINGEREZA WALIOMWAGIWA TINDIKALI WAKIMBIZWA KWAO KWA MATIBABU ZAIDI. RAIS JAKAYA KIKWETE AWAJULIA HALI KABLA YA KUONDOLEWA

unyama 566d1

Friday, August 9, 2013

Milioni 10 kwa taarifa za washukiwa Zanzibar

Kristie Trup na Katie Gee
Polisi nchini Zanzibar wameahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni 10 za Tanzania kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa watu waliowashambulia wasichana wawili waingereza kwa Tindikali.
Wasichana hao kutoka London, Kirstie Trup na Katie Gee, walirushiwa Tindikali kwenye nyuso zao walipokuwa wanatembea mjini Jumatano Jioni.
Polisi wanasema kuwa hizo ni pesa nyingi sana kisiwani Zanzibar.Serikali ya Zianzibar ndio itakayotoa zawadi hiyo.
Kirstie Trup na Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18 kutoka London, walipelekwa hospitalini nchini Tanzania baada ya kushambuliwa Mashariki mwa kisiwa hicho.
Inaaminika kuwa walitoka Tanzania kuelekea Uingereza Alhamisi usiku.
Mama za wasichana hao, Rochelle Trup na Nicky Gee, walielezea kughadhabishwa mno na shambulizi hilo ambalo sababu yake haiwezi kujulikana na ambalo halikuchochewa kivyovyote. Walishambuliwa na wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki.
Polisi walisema kuwa walirushiwa Acid kwenye nyuso zao, kifuani na kwenye mikono yao walipokuwa wanatembea mjini .
Mwandishi wa BBC anasema kuwa waliowashambulia walitoroka na polisi hawajui kwa nini wanawake hao walilengwa.
Mama za wasichana hao walisema kwenye taarifa yao kuwa walighadhabishwa mno na shambulizi hilo na hawaelewi kwa nini wasichana hao walishambuliwa ili hali walikwenda Zanzibar kwa nia njema.
''Tunashukuru kwa wale wanaotaka kujua kinachoendelea lakini tungeomba vyombo vya habari vituwache kwa sasa hadi tutakapokutana na watoto wetu,'' alisema msemaji wa familia za wasichana hao.
Wasichana hao walikuwa wamekaa Zanzibar kwa muda wa wiki mbili ingawa walitarajiwa kuwa huko kwa wiki tatu, kupitia kwa kampuni ya usafiri ya i-to-i Travel, ambayo ilisema inafanya kila iwezalo kuwarejesha nyumbani Uingereza.
Kari Korhonen, mkurugenzi mwenza wa kampuni ambayo wasichana hao walikuwa wanafanyia kazi, alisema kuwa hali yao si mbaya ikizingatiwa athari za Acid kwa mwili na visa ambavyo vimewahi kushuhudiwa vya kuchomwa kwa Tindikali
Msemaji mwingine aliongeza kuwa wasichana hao walikuwa njiani kuelekea kwa maankuli ya jioni wakati wa shambulizi hilo.

Nini maana nyingine ya 'Bongoland'?



Mwanasiasa Godfrey Bloom

Chama cha kibinfasi cha kisiasa cha MEP nchini Uingereza kimeshutumiwa kwa kutumia neno.......'Bongo Bongo Land'
Lakini kwa baadhi ya watu nchini Tanzania, neno hilo lina maana isiyo na ubaya wowote.
'Bongo Bongo land' ni neno ambalo hutumiwa miongoni mwa waingereza kama lugha ya dharau kuashiria nchi maskini, au mataifa yanayostawi.Mwanachama wa chama hicho, Godfrey Bloom, amenukuliwa kwenye jarida la Guardian akisema,'' inawezekanaje tunatoa msaada wa pauni bilioni moja kila mwezi, kwa 'Bongo Bongo Land' wakati tunakabiliwa na deni kubwa kama hili?''
Bloom aliambia BBC kuwa Bongo Bongo Land ni neno wanalotumia watu kuashiria nchi maskini isiyo na ustaarabu.
Hili bila shaka halikumfurahisha Laura Pidcock, mwanaharakati anayepinga ubaguzi wa rangi aliyesema kuwa dhana hizi ambazo watu wanazo kuhusu watu fulani, inarejesha Uingereza nyuma wakati inajipa sifa ya kuwa nchi yenye ustaarabu.
Alisema dhana kama hizo zinapotosha sana.
Wakereketwa wamemtaka kukoma kabisa kutumia tena lugha kama hiyo wakisema kuwa watu katika mataifa ya kigeni watatizama hilo kama ubaguzi wa rangi.
Haya yote yatakuwa habari muhimu kwa watanzania ambako neno hili kwa kifupi,Bongoland lina maana tofauti kabisa na ilivyotafsiriwa na mwanasiasa huyo.
Badala yake inamaanisha mahala ambapo watu wanapaswa kuwa wajanja na kuwa makini wakati wote.
Sehemu hiyo, ni mji mkubwa wa Dar es Salaam. Linatokana na mchanganyiko wa neno la Kiswahili Ubongo - lenye maana Akili,
na neno - land.

Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau anafafanua . "Dar es Salaam ni sehemu ambapo watu hawana budi ila kutumia akili zao. Unaweza kuwa tapeli au mfanyabiashara lakini lazima wawe na mbinu ya kupata pesa.''
Neno hili unaweza kusema ni jipya...kulingana na Famau...limekuwa likitumika kwa miaka 15 sasa. Babake hawezi kuwa analitumia , linatumika sana miongini wa vijana walio chini ya umri wa miaka 35. Lakini linasifika sana kiasi cha kuwahi kuwa jina la filamu iliyotolewa mwaka 2003 kuhusu kijana mmoja mtanzania kuhamia Marekani na fimalu hiyo ikawa na sehemu yake ya pili kwa Bongoland II.
Cha mno zaidi, ikiwa utatumia neno Bongoland nchini Tanzania basi unakuwa umegonga ndipo na kwa hilo unapata pointi hapo wala sio kukosolewa,'' anasema Famau.
Labda ufafanuzi huo ungemsaidia bwana Bloom kujizuia na utata aliosababisha.
http://www.bbc.co.uk/swahili

Dk. Richard: Fedha ni hatari kwa afya yako

Bofya hapa kusoma habari kamili









Sikiliza hii

Ndege ya kijeshi yalipuka Mogadishu

Ndege ya kijeshi imelipuka na kuteketea nchini Somalia baada ya kutua kwa dharura katika uwanja wa kimataifa wa ndege mjini Mogadishu.
Kikosi cha muungano wa Afrika nchini Somalia ambacho kina kambi yake katika uwanja huo wa ndege kimesema kuwa wanajeshi wake kadhaa wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa.
Inasemekana kuwa ndege hiyo ilikuwa ya jeshi la Ethiopia.
Kuna ripoti kuwa ndege ilikuwa imebeba zana za kivita.
Wafanyakazi katika uwanja huo wa ndege walielezea kusikia milipuko kadhaa huku moto ukienea kwa ndege hiyo.
Ndege za kijeshi hutua katika uwanja huo wa ndege unaotumiwa na wanajeshi wa muungano wa Afrika wanaopambana dhidi ya wapiganaji wa Al shabaab wanaosemekana kuwa na uhusiano na al Qaeda.
Wakati huohuo, kwenye mtandao wao wa Twitter kundi la Al Shabaab limeeleza kufurahia kwa kulipuka kwa ndege hiyo hasa kwa kuwa ililipuka yenyewe.
Kwenye ujumbe mwingine , kundi hilo lilisema kuwa ndege hiyo iliyokuwa imebeba silaha iliteketea katika uwanja wa Mogadishu na kuharibu kila kilichokuwa kwenye ndege yenyewe.
Kundi hilo lililaumu ilichokiita watu waliolaaniwa kwa kupanga mauaji ya waumini na kufanya uharibifu lakini kila wanachokifanya, juhudi zao zinagonga mwamba.

http://www.bbc.co.uk/swahili

Thursday, August 8, 2013

Afueni kwa wasafiri wa ndege Kenya



Shughuli katika uwanja wa kimataifa wa ndege JKIA nchini Kenya, zinatarajiwa kurejea katika hali ya kawaida kuanzia usiku wa manane.

Waziri wa usafiri, Michael Kamau, amesema kuwa sehemu iliyotengewa marasia kuingilia na kutoka kwenye uwanja hyuio itatumiwa na wageni kutoka nchi za kigeni watakaowasili katika uwanja huo.

Ndege za kimataifa zimeanza kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa jijini Nairobi JKIA, siku moja tu baada ya kitengo cha kuwasili wageni kuchomwa na moto mkubwa na kulazisha uwanja huo kufungwa kwa masaa kadhaa.Safari kadhaa za ndege za kimataifa zilirejea leo huku ndege za shirika la ndege la Kenya zikitua na kuruka katika hali inayoweza kusemekana kuwa ya kawaida.

Ndege ya kwanza ya kimataifa kuwasili katika uwanja huo ni ile iliotoka Uingereza na baadaye nyengine kutoka Tanzania na Bangkok zikawasili.

Wachunguzi hata hivyo wanatathmini chanzo chake.

Wakati huo huo Rais wa Marekani, Barack Obama amesema ataisaidia serikali ya Kenya katika kukarabati uwanja huo wa ndege baada ya moto mkubwa kuuteketeza hapo jana.

Katika ujumbe wake wa simu, Obama alisisitiza kuwa Marekani iko tayari kuisadia Kenya katika hali ile yoyote kutokana na ushikiano wake na Kenya.

Obama pia aliwapa pole familia zilizowapoteza wapendwa wao katika mashambulizi ya bomu ya Agosti 1998 mjini Nairobi.

Manmo Jumatano, moto mkubwa uliotokea majira ya asubuhi, uliharibu kitengo cha kuwasilia wageni wa kimataifa.


Vikundi vya wachunguzi viliwasili katika uwanja huo kufanya uchunguzi wao kubaini kilichosababisha moto huo.

Abiria walikwama kutokana na mkasa huo ingawa waliweza kuondolewa nje ya uwanja kwa ajili ya usalama wao huku baadhi wakiangalia mizigo yao ikiteketea wasijue la kufanya.

Rais Uhuru Kenyatta aliwasili katika uwanja huo na kujionea uharibifu uliotokea na kiisha kutoa taarifa yake kupitia kwa msemaji wake Esipisu aliyesema kuwa chanzo cha moto huo kinachunguzwa.

WANAWAKE WAINGEREZA WASHAMBULIWA ZANZIBAR


Maji ya AcidPolisi katika kisiwa cha Zanzibar wamesema wanawake wawili wa Uingereza wamerushiwa maji ya Acid katika nyuso zao baada ya kuvamiwa mwendo wa usiku.
Naibu kamishna wa polisi amesema kuwa wanaume wawili waliwatendea wanawake hao kitendo hicho walipokuwa wakitembea katika barabara za mji wa kihistoria wa zanzibar.
Amesema kuwa polisi tayari wameanzisha msako dhidi yao wanaume hao.
Wanawake hao, wanasemkana kufanyia kazi shirika moja la kujitolea na nia ya shambulizi hilo haijulikani.Polisi wanasema kuwa wanawake hao wenye umri wa miaka 18 walikuwa wakitembea katika mji wa Mawe kisiwani Zanzibar ambao ni kivutio kikuu cha utalii kisiwani humo, wakati wanaume wawili waliokuwa wamepanda piki piki walipowamwagia Acid kwenye mikono , vifua na nyuso zao.
Wanawake hao wanaoaminiwa kuwa ni wahudumu wa kujitolea wa shirika la misaada, walipelekwa kwa ndege hadi Dar es Salaam ambako wanapata matibabu . Afisa wa wizara ya afya amesema kuwa majeraha yao si ya kutishia maisha .

Monday, August 5, 2013

MDC chatishia kwenda mahakamani

Siku moja baada ya Rais Robert Mugabe na Zanu PF kutangazwa kushinda uchaguzi Mkuu nchini humo, baadhi ya wafuasi wa upinzani kutoka chama cha MDC wanasema wameshambuliwa na wenzao wa ZANU PF.
Baadhi ya dola za Magharibi ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, zimetilia shaka iwapo uchaguzi huo ulifanyika kwa uwazi.
Madai hayo yanakuja siku moja baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi uliofanyika Jumatano kutolewa na kumpa ushindi rais Robert Mugabe. Chama chake Zanu-PF kilipata thuluthi tatu ya viti vya bunge.
Watu 11 mjini Harare na wengine 20 kutoka mkoa wa Mashonaland, wanasema kuwa walishambuliwa na wafuasi wa Zanu-PF wanaojulikana sana baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Chama cha MDC kimesemna uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya wizi wa kura.
Kiongozi wake Morgan Tsvangirai, ameahidi kuchukua hatua za kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi.
Pia alisema kuwa chama chake cha MDC, hakitashirikiana na kile cha Mugabe na kuwa kitasusia kushikilia nafasi zozote katika taasisi za serikali.
Vyama hivyo viwili, vimekuwa wanachama wa serikali ya Muungano tangu mwaka 2009,baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2008 kusababisha ghasia.
Watu 11 waliodai kushambuliwa katika mtaa mmoja mjini Harare waliomba hifadhi katika makao makuu ya chama cha MDC mnamo Jumapili, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Brian Hungwe.
Wanadai kuwa walishambuliwa na wafuasi wa Zanu-PF waliokuwa wanakwenda nyumba hadi nyumba wakiwaamuru wafuasi wa MDC kufunga virago vyao na kuondoka.
Kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai alisema uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya wizi.
Msemaji wa MDC, Douglas Mwonzora, alisema kuwa mashambulizi hayo yalipangwa. Lakini msemaji wa chama cha Zanu PF, Psychology Maziwisa, alikanusha madai kuwa wafuasi wa chama walikuwa wanawashambulia wapinzani wao.
MDC kinaonya kuwa hakitaweza kuwadhibiti wafuasi wake ikiwa madai ya wao kushambuliwa yataendelea.
Chama hicho kimeomba muungano wa nchi za Kusini mwa Afrika , Sadc, kuingilia kati na kuzuia hali kuzorota zaidi kiasi cha kutoweza jkudhibitiwa.
Baadhi ya wakuu wa chama cha MDC, wametoa wito kwa wafuasi wao kutoitii serikali na kutenga chama cha Zanu-PF.