Sunday, July 29, 2012

Pichani Mh. Kabati akimkabidhi msaada wa jezi Francis Godwin, mratibu wa klabu ya mpira ya TASWA, Iringa. Franchis pia ni bloga mahiri na anamiliki blogu yake ya Francisgodwin.blogspot.com



Na Mwandishi wetu Iringa



Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Mhe. Rita Kabati (CCM) na mbunge wa jimbo la Ismani Wiliam Lukuvi wameanza kuisaidia jezi seti moja moja timu ya waandishi wa habari za michezo Tanzania (TASWA) mkoa wa Iringa kama njia ya kuiunga mkono timu hiyo katika kuhamasisha michezo mkoani Iringa.

Akikabidhi msaada huo leo kwa mwenyekiti wa TASWA mkoa wa Iringa Francis Godwin ,mbunge Kabati alisema kuwa amelazimika kutoa msaada huo kama sehemu ya kuunga mkono unzishwaji wa timu hiyo .

Kwani alisema suala la michezo lime katika ilani ya uchaguzi wa CCM hivyo akiwa kama mbunge ameguswa na mkakati wa wanahabari mkoa wa Iringa katika kuhamasisha michezo na kuwa miongoni mwa wadau wa kweli wa michezo ambao wamekuwa wakiandika habari za michezo ila pia na wao wenyewe kuonyesha mfano katika michezo kwa kuwa na timu yao.

Mbunge Kabati alitoa wito kwa wabunge wengine na wadau wa michezo katika mkoa wa Iringa kujitokeza kuisaidia timu hiyo vifaa vya michezo pamoja na misaada mbali mbali pale inapohitajika ili kuiwezesha kuwa timu bora katika mkoa wa Iringa.



Kabati alisema kuwa bado ataendelea kuisaidia timu hiyo ya TASWA pamoja na kuisaidia vifaa zaidi vya michezo kwani imeonyesha mfano mwema kwa makundi mengine ya kijamii katika mkoa wa Iringa.



Mbali ya kuahidi kuendelea kuisaidia timu hiyo bado alisema anaiandalia safari ya kwenda bungeni Dodoma ili kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuitambulisha rasmi kwa wabunge wa mkoa wa Iringa na wabunge wengine ila nao kuanza kuzisaidia timu kama hizo katika mikoa yao.



Hata hivyo alimpongeza mwenyekiti wa TASWA Iringa Francis Godwin kwa kuanzisha mkakati huo mzuri wa kuwa na timu ya pamoja na wanahabari wote itakayojenga umoja na mshikamano miongoni mwa wanahabari mkoa wa Iringa.



Mbunge Kabati alisema kuwa pamoja na kuisaidia jezi timu hiyo ya TASWA pia amekuwa akisaidia vifaa vya michezo timu mbali mbali za vijana katika jimbo la Iringa mjini na majimbo mengine yanayounda mkoa wa Iringa na kuahidi kuendelea kufanya hivyo kwa vijana wote ikiwa ni pamoja na kuwaahidi vijana hao kuwaunganisha kupitia tamasha kubwa la michezo ambalo litafanyika hivi karibuni mjini Iringa kwa vijana wa mkoa mzima wa Iringa.



Kwa upande wake mwenyekiti wa TASWA Iringa Francis Godwin akishukuru kwa msaada huo alisema kuwa mbunge huyo ameonyesha mfano kwa wabunge wengine na wadau wa michezo katika kuisaidia timu hiyo na kumwomba kuwa mlezi wa timu hiyo .



Godwin alisema kuwa mbali ya mbunge Kabati kusaidia seti hiyo ya jezi pia mbunge wa jimbo la Ismani Wiliam Lukuvi ambaye ni waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera na uratibu wa bunge pia ameisaidia timu hiyo jezi seti moja na kuwa jezi hizo zote zitakumbukwa na TASWA kwa kuandikwa majina yao nyuma ya jezi hizo kama njia ya kuwaenzi kwa mchango wao huo.



Hata hivyo alisema kwa sasa timu hiyo inakabiliwa na ukata wa fedha kwa ajili ya kusafirisha timu hiyo kwenda kucheza mechi za kirafiki na timu za nje ya mji wa Iringa ,pamoja na viatu vya wachezaji na hivyo kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuendelea kuisaidia zaidi.



Wakati huo huo Godwin alisema kuwa timu hiyo ya TASWA 2012 itazinduliwa rasmi siku ya jumapili katika uwanja wa Samora mjini Iringa kwa mchezo wa kirafiki kati ya waheshimiwa madiwani na wanahabari hao hivyo kuwataka wanahabari mkoa wa Iringa kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mazoezi yanayoendelea katika viwanja vya Kleruu kila siku majira ya saa 11 .30 jioni .

No comments:

Post a Comment