“WAKATI nahitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya ofisi yangu mwaka
jana, niliahidi kuwa Serikali itaangalia upya viwango vya posho za madiwani kwa
lengo la kuviongeza,” alisema Pinda na kuongeza;
“Sasa zoezi hilo limekamilika na kuanzia mwaka 2012/2013 madiwani watalipwa
viwango vipya vya posho vilivyoboreshwa.” Gazeti la Mwananchi la Jumatatu , tarehe
25 Juni mwaka huu, lilimkariri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitamka maneno
hayo, wakati akisoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi), kwa mwaka 2012/13.
Pinda ametangaza kuongeza posho za madiwani akijitetea kuwa anatimiza
ahadi yake ya mwaka uliopita wa fedha.Kufanya hivyo kwa Pinda ni kuwafurahisha
na kuwaridhisha madiwani hivyo kufanya waipende serikali na kuiabudu.
Wafanyakazi wengi wa serikali
wamekuwa wakilalamika juu ya mishahara midogo, posho ndogo au hakuna
kabisa; lakini hawapati wanacho lalamikia kwa serikali.
Maisha ya Mtanzania wa kawaida yamekuwa magumu kwa sasa, kiasi kwamba
hata familia zipo hatarini kusambaratika.Baba hana kitu na mama hana
kitu,watoto wanapiga miayo muda wote.
Kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitalini karibu kote nchini mara
kwa mara wauguzi/madaktari wanawajibu wagonjwa
kuwa hakuna dawa.Wakanunue madukani.
Kwenye shule za msingi za umma , ‘kaumba’, hakuna vitabu,chaki na
madawati ya kutosha. Wanafunzi wanakaa wanne mpaka watano katika dawati moja.
Walimu wanatoa fedha zao mifukoni kununua chaki, na wazazi wanaelezwa
kuwanunulia watoto wao vitabu kwani hali ni mbaya.
Fedha za rudhuku kwa maendeleo ya shule ni kitendawili.Katika baadhi ya
shule nchini hazifiki kabisa, kwingine zinachelewa kufika na zikifika zinakuwa
kidogo.
Mfano,ofisa mtendaji katika kata moja huko wilayani Mufindi alinieleza
kuwa katika kata yake, fedha ya rudhuku iliyoletwa katika baadhi ya shule ni
shilingi 20,000 tu, haitoshi hata nauli ya mtu anaetoka kijijini huko kwenda
mjini mafinga kununua vitendea kazi vya shule.
Hali hii ya maisha magumu katika jamii, ambayo ni ashirio la kudorora
kwa uchumi wa nchi, inawaumiza sana
wananchi maskini hasa ukizingatia hata huduma za kijamii zinazopaswa kutolewa
bure au kwa unafuu kama huduma za afya na elimu nazo hazitolewi kwa kuridhisha.
Wakati Pinda anatangaza kuongeza posho za madiwani, wabunge
walishangilia kwa kishindo.Nini maana yake?Mimi na wewe tujiulize.
Kadri siku zinavyosonga mbele hali ya uendeshwaji wa shule zetu za
misingi za umma inazidi kuwa mbaya.Walimu wamekosa matumaini ya kuishi na
kufanya kazi kwa moyo mmoja.
Wengi wamechakaa,wamepauka na kuonekana wazee wakati bado vijana
.Serikali ipo kimya,wanafunzi wanakosa vifaa muhimu, wanatimiza wajibu tu wa
kuwa shule, na kusogeza siku mbele.
Tumefikia kipindi shule zetu zinaendeshwa kwa fedha za michango ya
wananchi, walizochanga kwa ajili ya maendeleo mengine ya vijiji vyao.
Wenyeviti wa vijiji wameamua kutumia michango iliyochangwa kwa ajili ya
kazi nyingine ili kusaidia wanafunzi waendelee kupata elimu lakini bado
tunawalaumu kwa kufanya hivyo.
Mfano,mwezi uliopita iliripotiwa katika vyombo vya habari kuwa, ‘Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Gerald
Guninita amemkamata na kumweka chini ya ulinzi, Mwenyekiti wa Serikali ya
Kijiji cha Udekwa kilichopo Tarafa ya Mahenge, Obadiah Lubugo, kwa kutochangia
Sh.70,000 za Mbio za Mwenge’.
‘Lubugo, ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji
kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alionja kadhia hiyo
baada ya kuelekeza fedha hizo katika manunuzi ya chaki
kwenye Shule ya Msingi Udekwa’.Mwisho wa kunukuu.
Lubugo amejitetea kuwa alifanya hivyo baada ya kuona shule haina chaki
na wanafunzi hawasomi kutokana na kukosekana kwa chaki, lakini ameonekana
kapotoka na kukosea.
Lakini kulingana na hali halisi ilivyo sasa katika shule hizo za umma, alichofanya
mwenyekiti huyu, kutoa fedha za kijiji zilizokusudiwa kutumika kwa kazi
nyingine ili kununulia chaki na kufanikisha wanafunzi kufundishwa, kimekuwa
kikifanywa na wenyeviti wengine wa
vijiji mara kwa mara.
Tunakwenda wapi? Shule zinakosa chaki, sisi tunawaongeza madiwani posho.
CHANZO: KWANZA JAMII-IRINGA
|
No comments:
Post a Comment