Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Bi , Susan Rice,
amesema Marekani itaimarisha juhudi zake nje ya baraza la usalama la Umoja wa
Mataifa ili kushinikiza serikali ya Syria kuachia madaraka.
Bi. Rice, aliyasema hayo baada ya Urussi na Uchina kutumia kura zao za turufu
katika baraza hilo la Usalama kupinga vikwazo zaidi dhidi ya serikali ya Syria,
ikiwa haitasitisha utumizi wa silaha nzito nzito dhidi ya waasi na raia.
Urussi ilisema kuwa azimio hilo la baraza la usalama lililoungwa mkono na
mataifa ya Magharibi halikubaliki kwa sababu lingetekelezwa kwa kuwatumia
wanajeshi.
Msemaji wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Kofi Annan, Ahmad
Fawzi, alisema Bwana Annan, amesikitishwa sana na hatua hiyo ya Urussi na Uchina
ya kutumia kura zao za turufu kupinga azimio hilo.
Wakati huo huo wapiganaji wa upinzani nchini Syria wameuteka na kutwaa
uthibiti wa vituo kadhaa vya kuvuka mpaka kuingia nchini Iraq na Uturuki.
Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Iraq, amesema wapiganaji wa waasi wa Free
Syrian Army, wametwaa uthibiti wa kituo kinachotumiwa kuingia nchini humo kutoka
Syria.
Katika kituo kingine cha mpakani nchini Iraq, maafisa wa serikali ya nchi
hiyo wamesema wanajeshi wa waasi wamewauawa takriban wanajeshi 20 wa serikali ya
Syria.
Kituo muhimu cha kuingia Uturuki kutoka Sria cha Bab al Hawa pia kilitwaliwa
na waasi hao, lakini wameanza kuondoka.
|
No comments:
Post a Comment