Saturday, July 7, 2012

Takrima ilikufa, kivuli chake bado kipo

WIKI iliyopita nilizungumzia juu ya Tanzania tunayoitaka, ambapo kimsingi nilieleza sifa za viongozi ambao tunatakiwa kuwa nao katika taifa letu.
Pamoja na mambo mengi niliyoyaeleza katika makala hayo, pia nilisema tunahitaji kuwa na taifa lenye viongozi wanaowajibika, wenye kutenda haki, kujali haki za binadamu, kutumika kwa maslahi ya umma, wenye kukataa rushwa ndogo na kubwa, watakaotuongoza katika mafanikio ya kweli na watakaokataa kutumika kwa maslahi ya vyama vyao bali kwa maslahi ya Watanzania wote.
Leo katika safu hii nimeona ni vyema nikazungumzia kuhusu rushwa ambayo imekuwa ikihusisha wanasiasa na wananchi hasa katika kipindi cha uchaguzi.
Tutakumbuka kwamba katika miaka ya karibuni wawakilishi wetu walifikia hatua ya kubariki rushwa ambayo ilibatizwa jina la ghiliba la ‘takrima’.
Takrima ilikuwa ni kutoa ruksa kwa mwanasiasa anayegombea nafasi fulani ya madaraka hapa nchini; iwe urais, ubunge au udiwani kumpatia kitu kidogo mpiga kura kama njia ya kumshukuru.
Takrima hiyo ikaruhusu mtu kumshukuru mpiga kura wake hata kabla ya uchaguzi. Ilikuwa ruksa kumpatia pesa, nguo, chakula na zawadi nyingine yeyote mtu ambaye unadhani angeweza kukupigia kura.
Hata hivyo, takrima haikudumu kwa kipindi kirefu, wale wale waliofikiria na kuibariki walifikia uamuzi wa kuiondoa na kusema kuwa ni rushwa. Neno takrima likaishia hapo kutumika, lilikosa mvuto, lilitelekezwa na hakuna aliyelitumia tena.
Hali halisi ya mazingira ya kisiasa hapa nchini inaonyesha kuwa neno takrima lilikufa, lakini kivuli chake bado kinaishi.
Wengi mtakubaliana nami kuwa, fedha, sabuni, fulana, kofia, khanga bado zinatolewa bure kwa wananchi, iwe kipindi cha karibu na uchaguzi au katika uchaguzi wenyewe.
Hizi ni zawadi zinazotolewa na baadhi ya wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi hapa nchini kwa wananchi, ili tu wachaguliwe kushika nafasi za madaraka.
Wananchi wanaoishi kwenye lindi la umaskini, ambao watoto wao wanasoma kwenye vyumba vya madarasa vilivyoezekwa kwa nyasi, huku wabunge na madiwani wakitafuna posho za vikao bila hata mshipa wa aibu kuwashtua, wamekuwa wakidanganywa kwa khanga na fulana hadi kuamua kuwapa tena nafasi ya uwakilishi waheshimiwa hao hao.
Mbunge au diwani kuamua kutoa  zawadi za namna hiyo kwa wapiga kura wake ili wamchague tena ni ishara ya kuwa hakufanya kazi yake ipasavyo kipindi kilichopita.
Pamoja na majukumu mengine aliyonayo mbunge, anapaswa kuisimamia serikali ili iweze kuwajibika ipasavyo kwa wananchi ambao ndio wenye nchi. Madiwani pia wana jukumu hilo.
Hawa ni wawakilishi wetu, ndio wanaowakilisha Watanzania wote katika kuidai serikali haki zetu. Iwe huduma nzuri za kijamii, mfano; shule, hospitali na nyingine.
Kwa nini waidai serikali na wasifanye wao? Kimsingi katika utawala huu wa kidemokrasia, serikali na wananchi wapo katika uhusiano (relationship).
Kwa sababu ya uhusiano uliopo baina ya wananchi na serikali; serikali ikiwa mbeba majukumu na wananchi wakiwa ‘wenye haki’ (rights holders) ni lazima serikali iwajibike kwa wananchi.
Hivyo, serikali ndiyo baba na mama wa wananchi na mbunge na diwani ndio kaka mkubwa wa wananchi. Mbunge na diwani wanatakiwa kuwa katika sura ya mwananchi wa kawaida na kazi yao kubwa ni kumwambia baba na mama kuwa sisi huku tunataka shule, hospitali, barabara ni vitu vingine vingi. Siyo wao kuanza kutoa fedha zao na kufadhili wananchi kwa vitu vidogo vidogo ili wawaone ni watu wema.
Kutoa fulana, khanga, fedha na zawadi nyingine kwa wananchi ni  kutoa rushwa. Rushwa iliyogeuzwa kuwa uwajibikaji kwa wananchi na wao wakakubali na kushangilia kuwa mbunge au diwani anatujali.
Hiki ni kivuli cha takrima na jamii inapaswa kutambua kuwa hii ni rushwa na wala siyo uwajibikaji.

No comments:

Post a Comment