Monday, April 15, 2013

Damas: Mtunzi wa Nyamidela anayelia na ukosefu wa fedha


Na John Mnubi

“NILIANZA kugundua kuwa nina kipaji cha muziki tangu mwaka 1998 nikiwa darasa la sita huko mkoani Morogoro.”
Hayo ni maneno ya Damas Masonda anayetamba na kibao chake cha Nyamidela.
Alizaliwa mwaka 1984 mkoani Iringa katika Kijiji cha Mdabulo wilayani Mufindi, lakini akiwa na miaka mitano walihamia Morogoro kutokana na wazazi kutafuta maisha bora.
Alijiunga na elimu ya masingi mwaka 1993 ambapo mwaka 1999 alihitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Morogoro ambako aliishia kidato cha pili kutokana na wazazi kushindwa kuendelea kumsomesha.
Anasema kutokana na ugumu wa maisha, baada kuacha shule alijiingiza kwenye biashara ya uuzaji wa maembe sindano ambayo alikuwa akiyafuata mlimani Kigurunyembe akiyaweka kwenye sinia na kutembeza mitaani ili kujikimu.
Baada ya kusota na maisha magumu alipata wazo ambalo alihisi lingemfanya afanikiwe kimaisha kupitia muziki ndipo alipoanza kuchanganua ni wapi aende ili afanikiwe, akapata jibu la kwenda Mwanza ambapo angekutana na mtayarishaji wa muziki maarufu kama Kid Bway wa Tetemesha Records.
Anasema alidunduliza fedha na kupata nauli ambapo alipanda treni kuelekea Mwanza. Alifikia maeneo ya Mwaloni ambako aliweka maskani yake huku akimuulizia mtayarishaji huyo wa muziki.
Lakini nyakati za mchana, Damas alikuwa akifanya vibarua vya kuaniaka dagaa, malazi yake yalikuwa kando kando ya Ziwa Victoria, maarufu kama Mwaloni.
“Baada ya kumtafuta kwa muda wa wiki mbili nilifanikiwa kukutana na vijana wenzangu wawili wenye kundi lao liitwalo Wabuza kutoka Sengerema ambao nao walikuwa kwenye harakati kama za kwangu ambapo tulifanya wimbo mmoja na Kid Bway lakini haukufanya vizuri,” anasema Damas.

Mafanikio
“Binafsi nimewahi kutunga na kuimba nyimbo karibu 14 lakini ninazojivunia kati ya hizo ni Mautamu iliyoandaliwa na prodyuza Hassy Kiss na hivi karibuni nimeachia kibao cha Nyamidela kilichotengenezwa katika studio za Shega Records jijini Kampala, Uganda,” anasema.
Anasema wimbo huo wa Nyamidela, ambao una mchanganyiko wa lugha mbili za Kihehe na Kiswahili, umefanikiwa kukakamata chati za juu kwa wiki kadhaa mfululizo katika kituo cha Radio Ebony FM kilichopo mjini Iringa.
Aidha, alifanikiwa kutengeneza video ya wimbo wake wa Mautamu, ambayo imetengenezwa na A Touch of Kalabani Video iliyopo jijini Dar es Salaam na tayari amekwishaisambaza kwenye vituo mbali mbali vya televisheni jijini Dar es Salaam ambako inachezwa.
“Katika kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia niliamua kuuweka kwenye mtandao maarufu wa www.youtube.com wimbo wangu wa Mautamu ambao nimeufanyia video ili dudia nzima waweze kuuangalia,” anasema Damas.
Aidha, Damas amefanikiwa kukutana na wasanii na watayarishaji wengi wakubwa wa muziki kupitia sanaa anayoifanya jambo ambalo limempanua upeo na kujifunza mengi kuhusu muziki.

Nyamidela
Anasema katika wimbo wa Nyamidela, ambalo ni neno la Kihehe likimaanisha ‘Matembele’ kwa Kiswahili, kwa kiasi kikubwa ameimba kuhusu wanawake wanaojiremba na kufanya ukware na kutembea na waume za watu, hatimaye kuvunja ndoa za wenzao na kuwaasa kuachana na tabia hizo ambazo si njema katika jamii na badala yake kila mmoja abaki na wa kwake.

Changamoto
Miongoni mwa changamoto zinazomkabili Damas ni kukosa kualikwa kwenye matamasha mbali mbali hata yale madogo yanayofanyika mkoani Iringa. Anasema amekuwa akikosa morali ya kufanya vitu bora zaidi kutokana na kukosa mialiko ambayo ingemtia moyo na kumuongezea kipato cha kujikimu na maisha.
“Tangu nianze muziki sijawahi kushika pesa taslimu ambayo naweza kusema nitaiwekeza au itanisaidia kujikimu na maisha zaidi ya kuambulia umaarufu tu na kujulikana na watu wengi, basi,” anasema.
Anasema anakabiliwa na hali ngumu linapokuja suala la kusambaza kazi zake ambapo hutumia nguvu nyingi kufanikisha suala hilo kwa sababu hana msimamizi wa kazi zake, yaani meneja.
“Nashindwa kufanya video kwa sababu unakuta wimbo umekubalika redioni, lakini sina fedha mfukoni, maana fedha inahitajika ili kufanikisha hilo. Bado nalia na kukosa mialiko kwenye matamasha maana nikialikwa nitapata fedha ya kutengeneza video nzuri,” anasema.
Kutokana na kuanza kuisambaza kazi ya Nyamidela kijijini kwake Nyabula, alivamiwa na kupigwa nyundo kichwani na kulazwa miezi mitatu mwishoni mwa mwaka 2012 akidai ni tukio lililotekelezwa na baadhi ya wanakijiji wenye wivu ambao hawakupenda mafanikio yake hasa walipokuwa wakisikia kibao chake kikipigwa karibu kila kona kijijini hapo.

Matarajio yake
Mara baada ya kupata fedha anatarajia kufanya video ya wimbo wake wa Nyamidela ambapo ataifanyia mkoani Iringa ikiwa ni njia moja wapo ya kuutangaza mkoa huo, lakini pia ujumbe na lugha iliyotumika kwenye wimbo huo kuwagusa zaidi wakazi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla.

Wito
Anasema waandaaji wa matamasha mjini Iringa na Tanzania kwa ujumla waweke mkazo kuwaalika wasanii wazawa kama njia mojawapo ya kuinua vipaji vyao.
Aidha, aliwaomba wakazi wa Iringa kupenda vya kwao na kuachana na kasumba ya kupenda vitu kutoka magharibi.

No comments:

Post a Comment