Monday, September 23, 2013

Milio ya risasi yasikika ndani ya Westgate

Huku hali ya mshikemshike ikiendelea kushuhudiwa katika jengo la Westgate lenye maduka, ufyatulianaji risasi umesikika ndani ya jengo hilo lenye maduka na mikahawa zaidi ya themanini.


Wapiganaji wa Al shabaab wamewateka nyara raia ambao idadi yao haijulikani. Walikuwemo ndani ya jengo wakiendelea na shughuli zao kuanzia Jumamosi mchana wakati wapiganaji wa Al shabaab walipowavamia na kuanza kufyatua risasi kiholela.

Inaarifiwa kuna maiti kumi katika ghorofa ya kwanza ya jengo hilo.


Inaarifiwa wapiganaji hao wanaoaminika kuwa wanachama wa Al Shabaab ni kati ya kumi na kumi na watano na bado wangali ndani ya jengo hilo.


Ripoti zinasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa risasi umesikika katika jengo hilo kwa takriban dakika 15.

Harakati za kuendelea kumaliza operesheni hiyo zinaendelea lakini hali ya mateka walio ndani ya jengo hilo inaendelea kudorora.


Wakenya waliofanikiwa kuondoka katika jengo la Westgate kwa usaidizi wa polisi

Rais Kenyatta amesema kuwa jueshi linajitahidi kuhakikisha kuwa linakabiliana vilivyo na wanamgambo hao.

Helikopta za polisi zinazunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi kushika doria. Vikosi vya usalama vinaendelea na operesheni kujaribu kuwanusuru waathiriwa wakati hali ikiwa ni ya ati ati katika eneo la shambulizi.


Awali jeshi la Kenya lilisema limeweza kudhibiti jengo hilo lote ingawa bado limetaja hali kuwa tete mno hasa katika kujaribu kuwaokoa mateka waliosalia ndani ya jengo hilo.


Ripoti zinasema kuwa watu 69 wamefariki katika shambulizi hilo la Al Shabaab kufikia sasa huku 175 wakijeruhiwa. Baadhi wametibiwa na kuondoka hospitalini. Baadhi ya majeraha waliyopata ni majereha ya risasi na kutokana na guruneti ambalo Al shabaa waliwarushia wale waliokuwa ndani ya mikahawa siku ya Jumamosi.


Kundi hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo kutokana na hatua ya kenya kupelekeka majeshi yake nchini Somalia ili kukabiliana na wapiganaji hao.

http://www.bbc.co.uk


Friday, September 20, 2013

WAZIRI KABAKA AZINDUA RASMI MCHAKATO WA MAANDALIZI YA USHIRIKI WA WAJHASIRIA MALI

Waziri wa Kazi na Ajira  Mhe. Gaudentia  Kabaka  leo  tarehe  19/09/2013, amezindua  rasmi  mchakato wa  maandalizi ya ushiriki wa Wajasiria mali wa Tanzania  katika Maonesho ya 14 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yajulikanayo  kama  Nguvu kazi/Jua kali.

Maonesho hayo yaliyoanza kufanyika  mwaka  1999 jijini Arusha  Tanzania wakati wa kusainiwa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yameendelea kufanyika kila mwaka kwa mzunguko katika nchi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Dhumuni kuu la maonesho haya ni kuwezesha sekta  isiyo rasmi kukua na kurasimisha shughuli zao katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwapatia fursa Wajasiriamali wa sekta hii kuonesha bidhaa zao, kukutana na wenzao, kubadilishana taarifa, ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na huduma pamoja na kuwezesha kupanuka kibiashara.

Jumla ya Wajasiriamali 1,070 kutoka nchi tano za  Jumuiya ya Afrika Mashariki wanategemewa kushiriki na Tanzania inatarajiwa kupeleka washiriki 250.

Mhe. Waziri Kabaka amesema,ili kurahisisha na kuharakisha ushiriki wa Wajasiriamali wa Tanzania katika maonesho hayo, kuna swala la usajili, na fomu za usajili pamoja na vigezo vya kuangalia kabla ya kujaza fomu ambavyo vinapatikana kwenye  Tovuti ya Wizara ambayo  ni www.kazi.go.tz

IMETOLEWA
Ridhiwan.M.Wema
Msemaji
WIZARA YA KAZI NA AJIRA.
19/09/2013

Hakimu achomwa kisu mahakamani


Wauguzi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga wakimuhudumia hakimu Satto Nyangoha aliyechomwa kisu shavuni jana, akiwa mahakamani na mlalamikaji katika kesi ya wizi wa baiskeli, Emmanuel Izengo. Picha na Suzy Butondo
Shinyanga. Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga, Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.
Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel Makelezia, mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia kuwepo mahakamani.
Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye thamani ya Sh150,000.
Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi yake ikiendelea na pande zote mbili zilitoa maelezo.
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi hiyo kusikilizwa mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo jana.
Kushambuliwa
Baada ya hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani na kuwashika mikono wote waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.
Ilidaiwa kuwa baada ya dakika 15, Izengo alirudi mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta risiti ya kumwonyesha hakimu thamani ya baiskeli yake alipoingia ndani ndipo kelele za Mshauri wa Baraza, Mary Wamba zikaanza kusikika akisema: ‘Njooni jamani hakimu kavamiwa anapigwa’.
Baada ya watu waliokuwa karibu kuingia katika ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu ameshacwhomwa kisu katika shavu la upande wa kushoto huku akivuja damu nyingi huku mtuhumiwa huyo akiendelea kumshambulia. Baada ya tukio hilo, wasamaria wema walimpeleka hakimu huyo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alilazwa kwa matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya tukio hilo kusubiri hatua za kisheria dhidi yake.
http://www.mwananchi.co.tz/

Polisi wakosoa uchunguzi wa Marikana



Polisi nchini Afrika Kusini wameikosoa tume inayochunguza mauaji ya wafanyakazi thelathini na nne katika mgodi wa madini ya platinum huko Marikana Agosti mwaka uliopita kusema kuwa walidangaya.
Katika taarifa idara ya polisi imesema kuwa madai dhidi yao ni ya kuudhi na hayana msingi.
Mawakili katika tume hiyo ya Marikana wamelaumu polisi kwa kutoa ushahidi wa uongo kuhusu hatua ya kutumia risasi wakitaka ukubalike bila upinzani.Wamesisitiza kuwa walitumia risasi kujilinda walipokuwa wakijaribu kuwatawanya na kuwapokonya silaha wafanyikazi hao waliokuwa wakigoma.

Baada ya kuchunguza kwenye Kompyuta za polisi walisema kuwa polisi walikuwa wamezuilia na kubadilisha yaliyokuwemo katika stakabadhi hizo.
Tume hiyo kwa mara nyingine imeakhirisha vikao vyake inapopitia maelfu ya stakabadhi zinazohusiana na tukio hilo.
Sasa polisi wanasema kuwa wamekuwa wakishirikiana na tume hiyo ya Marikana kikamilifu bila vikwazo vyovyote. Kadhalika wanataka wapewe nafasi kujieleza kabla ya mawakili kutoa hukumu.
http://www.bbc.co.uk/swahili

87 WAUAWA NA BOKO HARAM NIGERIA

tahmasebi20130917235522900_0a797.jpg
Wapiganaji wa Boko Haram wamewaua watu 87 katika shambulio katika Jimbo la Borno nchini Nigeria.
Mashahidi wanasema kuwa wapiganaji hao waliteketeza nyumba kadhaa katika tukio hilo la kutisha mnamo Jumanne usiku.
Shambulio hili limetokea siku chache baada ya makabiliano makali kati ya jeshi na wapiganaji wa Boko Haram
Wanamgambo hao waliokuwa wamevelia magwanda ya jeshi, waliweka vizuizi barabarani nje ya mji wa Benisheik na kuwapiga risasi wale waliokuwa wanajaribu kutoroka.(P.T)
Kwa mujibu wa taarifa za mashahidi , wapiganaji hao waliteketeza nyumba katika shambulizi hilo la Jumanne.
Kundi la Boko Haram, ambalo linapigania linachosema ni taifa la kiisilamu nchini Nigeria, limekuwa likifanya mashambulizi sawa na haya kuanzia mwaka 2009.
Jeshi linadai kuwa Agosti mwaka huu, kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau na naibu wake Momodu Bama waliuawa , ingawa hakuna taarifa za kujitegemea kuthibitisha hilo.
Mawasiliano katika jimbo la Borno, yamekumbwa na hitilafu, tangu mwezi Mei, wakati hali ya hatari, ilipotangazwa katika jimbo hilo na majimbo mengine mawili.
Lakini mashambulizi yameongezeka sana hivi karibuni tangu jeshi kuanza kukabiliana na kundi hilo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Tuesday, September 3, 2013

MNARA WA DAUD MWANGOSI HUU HAPA

601_n_c3006.jpg
Leo Nyololo kwenye uzinduzi wa mnara wa kumbukumbu ya mauaji ya Daudi Mwangaosi, Kulia ni Benson Kigaila,wapili kutoka kulia ni Mdogo wake marehemu mwangosi,anayefuata ni Winfrida,na wa kwanza kutoka kushoti ni naibu katibu mkuu,Chadema Zanzibar Hamad Yusuf.(P.T)
Kwa hisani ya Mjengwa Blog.

Monday, September 2, 2013

KUMBUKUMBU YA MAREHEMU DAUDI MWANGOSI , MAANDAMANO YA WANAHABARI YATIKISA MJI WA IRINGA


Wanahabari  wa  vyombo  mbali mbali na  wadau  wa habari  mkoa  wa  Iringa  wakiwa katika  maandamano ya amani ya  kumuenzi  aliyekuwa mwenyekiti  wa klabu ya  waandishi  wa  habari  mkoa  wa Iringa (IPC) leo 
Maandamano  ya  wanahabari na  wadau  wa  habari yakipita  eneo la soko kuu la manispaa ya  Iringa 
Katibu  wa IPC  Francis  Godwin  akiongoza  maandamano ya  wanahabari na  wadau huku akiwa  juu ya gari na picha ya marehemu Daudi Mwangosi
Wanahabari  Iringa katika maandamano ya  kumuenzi  marehemu  Mwangosi  leo
 Maandamano ya  wanahabari  na  wadau  wa habari  mkoa wa Iringa ya  kumuenzi marehemu Daudi Mwangosi  yakipita  eneo ya  uhindini  


 Wananchi  wakishuhudia maandamano  hayo  leo





Katibu  mtendaji  wa IPC  Francis  Godwin akitoa taarifa ya  kuanza kwa maandamano ya kumuenzi marehemu Daudi Mwangosi leo
Katibu  wa  IPC Francis  Godwin mwenye pama akikabidhi maandamano ya  mwenyekiti  wa IPC Frank Leonard na  wadau  wengine  eneo la Maktaba ya  mkoa wa Iringa


Katibu  wa  IPC  FrancisGodwin kushoto akikabidhi picha ya marehdemu Daudi Mwangosi kwa  mwenyekiti  wa IPC  Frank Leonard kulia,wanaoshuhudia ni mzee  Fulgence  Malangalila  na Majid Mjengwa 


Mwenyekiti wa  IPC Frank Leonard  kushoto akikabidhi  picha ya  Mwangosi kwa mwasisi  wa IPC mzee Fulgence Malangalila 









MAANDAMANO ya  wanahabari  mkoa  wa  Iringa  kwa  ajili ya  kumbukumbu  ya  mwaka  mmoja wa  kifo  cha  aliyekuwa  mwenyekiti  wa klabu ya  waandishi  wa habari  mkoa  wa  Iringa (IPC) na mwandishi  wa Chanel  Ten Marehemu  Daudi Mwangosi  yatikisa mji  wa  Iringa leo.

Maandamano  hayo ambayo  yameanza majira ya saa 4 asubuhi  katika  viwanja   vya  bustani ya  Manispaa ya  Iringa yamepata  kuzungukakatika maeneo  mbali mbali ya  mji wa  Iringa kabla ya  kupokelewa na mwenyekiti  wa IPC  Frank Leonard katika  ukumbi wa maktaba ya  mkoa kwa mkutano wa  wadau  wa habari.

katika  maeneo  mbali mbali  ambayo maandamano  hayo yamepita  likiwemo  eneo la Uhindini , Mashine  tatu, Soko  kuu na stendi  kuu ya mabasi ya mikoani  wananchi  walilazimika  kusitisha  shughuli  zao kushuhudia maandamano  hayo ambayo yaliongozwa na  askari  wa  usalama barabarani .

CHANZO: www.francisgodwin.blogspot.com

Sunday, September 1, 2013

WARAKA WANGU KWA JWTZ, WATANZANIA

JWTZ 2 5c083
Na Manyerere Jackton, JAMHURI

Meja Khatibu Mshindo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amekufa katika mapambano nchini DRC. Amekufa kishujaa.
Amekufa akitekeleza maelekezo halali ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayolenga kuwafanya wananchi wa Mashariki mwa DRC waonje tunu ya amani.

Kifo cha kamanda huyu kinapaswa kiwe chachu kwa Watanzania na wapenda amani katika Afrika na duniani kote.(P.T)

Watanzania tuna historia iliyotukuka ya ukombozi wa wanyonge sehemu mbalimbali duniani. Ndugu zetu wa Msumbiji, Angola, Afrika Kusini, Namibia, Comoro, Ushelisheli, Angola na kwingineko wanatambua hilo. Bila kujali umasikini wetu, tulijitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanyonge katika mataifa hayo tunawakomboa. Wakati tukihaha kutekeleza dhima hiyo ya kiutu, hatukujali kuachwa nyuma kimaendeleo na majirani zetu kama Kenya au Malawi ambao hawakuhangaika kwa namna yoyote.
Kifo cha Kamanda Mshindo kinapaswa kiwe chachu kwa wapiganaji na makamanda wa JWTZ katika kuhakikisha wananchi wa DRC wanapata amani, wanafaidi matunda ya uhuru, na utajiri wao unabaki kuwanufaisha wao kwanza.
Tumempoteza Mtanzania mwenzetu katika vita ambayo mwasisi wake ni Rais Paul Kagame wa Rwanda. Huyu ni mpenda vita, na ndiyo chimbuko la kundi la waasi wa Kihutu la FDLR. Hili ni matokeo ya ubabe wake alipoamua kushiriki kuwaua Rais Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi, Cyprien Ntaryamira. Aprili 6, 1994 ndege iliyokuwa imewabeba viongozi hao kutoka nchini Tanzania ilipigwa kombora wakati ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Kigali, Rwanda.

Pamoja na marais hao, wengine waliouawa kwenye shambulizi hilo ni Bernard Ciza (Waziri wa Ujenzi wa Burundi), Cyriaque Simbizi, (Waziri wa Mawasiliano wa Burundi, Jenerali Deogratias Nsabimana (Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda), Meja Thaddée Bagaragaza (Msaidizi wa Rais wa Rwanda-masuala ya kijeshi), Kanali Elie Sagatwa (Mjumbe wa Sekretarieti ya Rais wa Rwanda), Juvénal Renaho (Mshauri wa Rais wa Rwanda wa Masuala ya Kigeni), na Emmanuel Akingeneye ambaye alikuwa Daktari wa Rais wa Rwanda.
Wana anga watatu, raia wa Ufaransa nao waliuawa. Nao ni Jacky HĂ©raud (rubani), Jean-Pierre Minoberry (rubani mwenza) Jean-Michel Perrine (mhandisi wa ndege).
Damu ya watu hawa inamsumbua Rais Kagame.
Taarifa mbalimbali kutoka pande mbalimbali duniani zinamweka mbele kwenye orodha ya waliohusika kwenye mauaji hayo ambayo baadaye yalisababisha kile kilichokuja kujulikana kama mauaji ya kimbari.

Dola ya Bahima
Watanzania tuna sababu zote za kupigana vita ndani ya DRC. Hii ndiyo njia pekee sahihi ya kuvuruga mkakati wa Rais Kagame na rafiki yake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda wa kuanzisha Dola ya Bahima. Hii ni dola ya watu wa kabila la Watutsi.

Marais hawa wanaamini Bahima inapaswa kusambaa Rwanda, Burundi, Uganda, sehemu za Tanzania na katika DRC. Tukiwaruhusu waimege DRC, nasi Tanzania tukae mkao wa kunyolewa! Hapa tunapaswa kutambua kuwa kwa huruma yetu tuliwakaribisha maelfu ya wakimbizi wa Kitutsi. Hawa wanajua mengi ya Tanzania. Haitashangaza siku moja wakijiunga na kuanzisha vita kwa madai ya kutaka watambuliwe. Tumeyaona juzi baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaamuru wahamiaji haramu warejee kwao.

Kumetolewa maneno mengi ya vitisho na lawama, kana kwamba ni halali kwa mtu kuishi katika nchi nyingine bila kufuata taratibu. Waliingia nchini mwetu wakiwa na mifugo mingi. Wakajitwalia maeneo makubwa kwa nguvu na kwa hila. Wakawaua wananchi wetu. Wakachoma nyumba na mashamba ya wenyeji. Kama wameweza kufanya hivyo sasa, watashindwa nini hapo baadaye kudai Karagwe na Ngara kuwa ni yao? Tuwe macho sana.
Rais Kagame alihakikisha anaingiza nchi yake kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, si kwa kutafuta kitu kingine, bali nguvu za kisiasa.
Chokochoko zake zimepamba moto baada ya ushauri wa Rais Kikwete wa kumtaka aketi na waasi ili wamalize tofauti zao kwa mazungumzo. Alichofanya Rais Kikwete ni kutoa ushauri, na si kumshurutisha! Kejeli, matusi na dharau vilivyotolewa baada ya kauli ya Rais Kikwete, vinaashiria kuwa kuna jambo kubwa zaidi ya hilo la kuchukizwa na ushauri aliompa.

Zipo sababu nyingi zinazomfanya Rais Kagame awe mbogo. Nitajaribu kuziainisha hapa kwa ufupi tu. Mosi, Tanzania tunakubalika sana kimataifa. Kwenye diplomasia tumeiacha mbali Rwanda. Hili linamuudhi sana kwani anaamini yeye ni bora na maarufu zaidi.

Kitendo cha Rais Barack Obama wa Marekani kuja Tanzania na kuziacha Rwanda, Uganda na hata Kenya kimewaudhi, na kwa kweli tunaweza kusema hii imekuwa nguzo imara iliyoibua mshikamano na mapenzi ya ghafla miongoni mwao. Rwanda ikijiona kuwa ndiyo nchi inayoinukia kiuchumi kwa kasi, ilidhani ina sifa zote za kuiwezesha kutembelewa na Rais Obama. Uganda ambayo ilikuwa mshirika mkuu wa Marekani, inaona Tanzania imechukua nafasi yake. Imeingiwa wivu! Kenya ambayo inaamini Obama ni wao kwa sababu babake ni Mkenya, imechukizwa kuona ikipigwa kumbo na Tanzania. Hawa watatu-Kagame, Museveni na Kenyatta-wameungana kuichukia Tanzania kwa sababu tu ya kumkosa Obama.
Pili, kinachomsumbua Rais Kagame na washirika wake ni uamuzi wa Tanzania wa kutaka Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC liende hatua kwa hatua. Msimamo wa Tanzania umekuwa kwamba maoni ya wananchi ni muhimu mno kabla ya kuchukua uamuzi wowote. Kwao, Tanzania ndiyo kikwazo cha kuwa na serikali moja ya EAC. Hapa ni vema Watanzania wakakumbuka namna Rais Museveni alivyokuwa amejiandaa kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki. Sidhani kama ameshaufuta mpango huo.
Baada ya kuona Tanzania tukitaka jambo hili liende hatua kwa hatua, watatu hawa wameungana sasa kutaka shirikisho lao la kisiasa, huku wakiiacha nje Tanzania na Burundi. Wanajidanganya bure. Lakini hapana sababu ya kulumbana nao. Kama wanataka kuanzisha, waanzishe tu. Hakuna haja ya ugomvi. Wakianzisha kutakuwa na nchi mbili-hiyo ya Shirikisho, na Tanzania kwa upande mwingine.
Hapa ni vema kwanza tukatambua kuwa Tanzania ni nchi kubwa. Ukichukua Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya, ukaziweka pamoja, bado ni ndogo kwa Tanzania. Hatuna sababu ya kuogopa.
Tatu, hawa jamaa kiu yao kubwa kabisa ni ardhi ya Tanzania. Ukiacha tamaa ya kutaka kuitawala kanda yote hii, kiu yao ya kweli ni ardhi ya Tanzania. Wamepambana kwa hali na mali kuhakikisha kuwa ardhi inakuwa moja ya mambo kwenye shirikisho. Wanataka Mkenya, Mganda, Mnyarwanda na mwanachama mwingine yeyote, akitaka kuingia Tanzania, basi apewe uraia wa kudumu na apata ardhi bila masharti!
Hoja yetu imekuwa kwamba wao wakija Tanzania watapata ardhi, je, Mtanzania akienda Rwanda au Kenya au Uganda ataipata? Chao chao, chetu chetu sote. Wao hawana mita ya mraba ya ardhi iliyo wazi kwa hiyo wanajua mlengwa na wa kuumizwa hapa ni Tanzania tu. Uroho wao wote ni ardhi ya Tanzania. Hilo tumeapa kuwa haliwezekani. Kama haliwezekani kwa ndugu wa tumbo moja, seuze kwa nchi na nchi? Tukianzisha shirikisho tutapeana nini? Hilo ndilo jambo wanalopaswa kutujibu kwanza. Janja ya kuja kuoa au kuolewa Tanzania haitawasaidia.
Wanachofanya sasa kinatokana na hasira tu
Shirikisho la Rwanda, Uganda na Kenya likianzishwa haliwezi kudumu. Watagombana tu. Rwanda watataka walitawale shirikisho. Hicho ndicho wanachokitafuta. Wakenya hawasumbuliwi na kingine, isipokuwa biashara. Wameingia kwenye mkakati huu kwa sababu wanadhani bandari ya Mombasa inaweza isiwe na maana endapo Rwanda, Uganda na Burundi wataamua kutumia bandari za Tanga na Dar es Salaam; na hiyo nyingine inayojengwa Bagamoyo. Bado ukweli unabaki kwamba kutoka Dar es Salaam hadi katika nchi za Rwanda na Burundi ni karibu mno kuliko kuanzia Mombasa.

Katika mpango huu sidhani kama Burundi itakubaliana nao. Burundi kuwa karibu na Tanzania kuna manufaa makubwa zaidi kwake kuliko kuwa karibu na hayo mafiga matatu.
Harakati hizi zote zinachochewa na Rwanda, na hapa ndipo ninapokuja na sababu ya nne ya Tanzania kuchukiwa. Rais Kagame amechukia mno kuona majeshi ya Tanzania yakiongoza mapambano ya kuwang'oa M23 ambao ni Wanyarwanda. Kwa miaka yote DRC imekuwa shamba la Rwanda. Kagame ameongoza harakati za kuliibia taifa hilo bila huruma. Ameanzisha vita ili amani isiwepo. Anajua DRC ikitawalika, hatapata mwanya wa kwenda kupora rasilimali, hasa madini. Kwa sasa adui yake mkubwa ni Rais Kikwete na Tanzania kwa sababu tunaziba njia yake haramu ya uchumi.

Kuachwa kwetu solemba EAC
Sioni kwanini tusianzishe Jumuiya yetu kwa kuwakaribisha DRC na Burundi. Sisi ni taifa kubwa. DRC ni taifa kubwa pia. DRC na Tanzania tuna rasilimali nyingi mno. Faida za kujitoa EAC ni kubwa kwetu kuliko kuendelea kuhangaika na hawa wapenda vita. Tuwaache waanzishe yao, na sisi tuanzishe yetu. La, hilo kama haliwezekani, tujikite zaidi SADC ambako kuna soko pana kuliko EAC.

Tukijitoa EAC atakayeumia zaidi ni Kenya maana bidhaa na uwekezaji wake mkubwa kauelekeza Tanzania. Soko lake kubwa lipo Tanzania. Wanajidanganya tu.

Tusiendelee kuwabembeleza watu wasiokuwa na shukrani. Tuwatakie heri katika ndoa yao hii mpya ambayo sioni uhai wake. Hizi ni hasira za mkizi ambazo mara zote humnufaisha mvuvi. SADC ni bora zaidi. Tupeleke nguvu zetu kwenye SADC.
Kagame na Museveni walisaidiana kuichukua Uganda. Museveni alimsaidia Kagame kuitawala Rwanda. Sasa wanasaidiana wachukue sehemu ya DRC. Museveni anamsaidia Kagame katika hili. Tutambue kuwa inayofuata ni Tanzania. Si ajabu wale Wanyarwanda waliokuja siku nyingi sasa wakadai wanabaguliwa, na kwa sababu hiyo wakaanzisha vita ya kutaka kutambuliwa au kujitenga na kuwa sehemu ya Rwanda na Uganda (Bahima Empire).
Njia pekee ya kumwondoa Rais Kagame ni hii aliyotusaidia kuiweka, yaani vita. Kuichokoza Tanzania ni njia ya kuelekea ukingoni mwa utawala wake. Amepigana kwa muda mrefu na wasiojua vita. Amejaribu kuitisha Tanzania akidhani atafanikiwa. Kinachotakiwa sasa ni kumwonyesha kazi. Safari iliyoanzia Goma inastahiki ihitimishiwe Kigali. Kama kasahau, arejee kwenye historia ili ajue kilichompata nduli Iddi Amin Dadaa. Buriani Kamanda Khatibu Mshindo.

Mwanamke ateuliwa waziri mkuu Senegal


Rais Macky Sall na mkewe wakati wa ziara ya Obama Senegal mwezi Juni

Rais Macky Sall wa Senegal amemteua mwanamke kuwa waziri mkuu mpya, masaa tu baada ya kumtoa kazini mwanasiasa aliyemteua aliposhika madaraka mwaka jana.
Aminata Touré, waziri wa zamani wa sheria, aliiambia redio ya taifa kwamba amekubali amri ya rais ya kuunda serikali mpya.
Bwana Mbaye, aliyewahi kufanya kazi kwenye benki, hakuwa mfuasi wa chama chochote cha kisiasa.Haikutolewa sababu ya Bwana Adbou Mbaye kutolewa kazini.
Bi Touré atakuwa mwanamke wa pili kuwa waziri mkuu nchini Senegal - baada ya Madior Boye, aliyeshika wadhifa huo kwa miezi 18 mwaka wa 2001.
Bwana Sall alimshinda Rais Abdoulaye Wade katika uchaguzi wa rais wa March 2012, akiahidi kupambana na umaskini na rushwa. )
http://www.bbc.co.uk/swahili