Uchapisha
wa Hati za Kusafiria (Pasipoti), nchini umesimama kwa muda baada ya
mashine zinazotumika kuharibika, Mwananchi limebaini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na
baadaye kuthibitishwa na Idara ya Uhamiaji, umeonyesha kuwa tatizo hilo
lilianza Januari na litaendelea hadi Mei mwaka huu.
Kusitishwa kwa huduma hiyo
kumesababisha mrundikano wa maombi ya hati hizo. Waombaji wanaopigwa
kalenda kupata hati hizo ni pamoja na wanaoomba kwa mara ya kwanza na
wale wanaotaka mpya baada ya za awali kujaa au kumalizika muda wake.
Kabla ya mashine hiyo kuharibika
muombaji aliweza kupata pasipoti yake ndani ya siku saba, baada ya
kukamilisha taratibu za uombaji, lakini kutokana na tatizo hilo,
imetimia miezi mitatu sasa, waombaji hawajui watapata lini hati hizo.
Baadhi ya waombaji walioongea na
gezeti hili walilalamikia kitendo hicho wakisema kinawasababishia
usumbufu na kuwakwamisha katika kufanya.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha
kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji na vishoka, tayari
wameanza kujinufaisha na tatizo hilo kwa kuomba rushwa kutoka kwa
waombaji hati hizo ili wawatekelezee matakwa yao kwa haraka.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Ndani Mbarak Abduwakil alikataa kuzungumzia suala hilo, akidai kuwa
amebanwa na vikao ofisini kwake.Hata hivyo, Kaimu Ofisa Uhusiano wa
Uhamiaji, Tatu Burhan alikiri kuwepo kwa tatizo hilo, lakini akasema
halitokani na mashine zao kuharibika.
"Tatizo hili limetokana na ukosefu wa
malighafi toka nje ya nchi. Unajua malighafi hizo tunaziagiza, lakini
kwa bahati mbaya hazikuweza kupatikana kwa wakati," alisema Tatu.
Pamoja na uhaba wa mali ghafi, alisema
kwa bado Uhamiaji iliendelea kutoa pasipoti kwa wenye maombi maalumu ya
dharura.Alikiri pia kwamba kwa waombaji wasio na dharura maombi yao
yaliwekwa kando yakisubiri kuwasili kwa malighafi.
Hata hivyo Tatu alisema kuwa mali ghafi hizo zimeshawasili Bandari ya Dar es Salaam jana na walikuwa katika harakati za kuzitoa.
"Hivi ninavyozungumza (jana) malighafi ghafi hizo tayari zimefika bandarani na tupo kwenye harakati za kuzichukua," alisema.
Alisema kuwa pamoja na malighafi hizo
kuwasili ni vigumu kuchapisha pasipoti zote kwa wakati mmoja kutokana na
wingi wa maombi.CHANZO MWANANCHI

No comments:
Post a Comment