Sudan Kusini imemfukuza afisaa mmoja wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa anachunguza
hali ya haki za binadamu.
Msemaji wa serikali anasema kuwa afisaa huyo alichapisha ripoti ya uchunguzi
wake ambayo haikuwa na ukweli
Maafisa wa umoja wa mataifa wamekosoa hatua hiyo wakisema kuwa ilikiuka
majukumu ya nchi hiyo ya kisheria.
Kufukuzwa kwa afisaa huyo, walisema kunaweza kuhusishwa na ripoti
iliyochapishwa mwezi Agosti na ambayo ilishutumu jeshi kwa kutesa, kufanya
ubakaji , mauaji na utekaji nyara.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wametoa madai sawa na hayo dhidi ya
nchi hiyo ambayo ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwezi Julai mwaka
jana.
Mchunguzi huyo wa umoja wa mataifa, alitajwa na maafisa wa umoja wa mataifa
kama Sandra Beidas.
Msemaji wa serikali Barnaba Marial Benjamin alisema kuwa afisaa huyo
aliripoti madai ambayo hangeweza hata kuthibitisha na amekuwa akizichapisha
ripoti zake bila sababu.
"Hili ni jambo linalokiuka maadili’’ alisema bwana Marial bila kufafanua
zaidi.
Hilde Johnson, mkuu wa ujumbe wa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Sudan,
aliitaja hatua hiyo ya kufurushwa kwa mjumbe huyo kama kuhujumu sheria ya
serikali chini ya makubaliano ya umoja wa mataifa.
Alisema kuwa alitaka serikali kutoa maelezo kuhusu hatua hiyo.
"Kuchunguza hali ya haki za binadamu na kuripoti na vile vile kuwezesha
mashirika ni mojawapo ya majukumu ya jeshi la UNMISS ambalo linapaswa kulindwa
," alisema afisaa huyo.
Mwezi jana shirika la, Amnesty International lilichapisha ripoti iliyotuhumu
wanajeshi wa serikali kwa kufanya vitendo vya kushangaza vya ukiukwaji wa haki
za binadamu ikiwemo mauaji na ubakaji.
Serikali ilijibu kwa kupuuza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu akisema
vilikuwa visa ambavyo havikutarajiwa.
|
No comments:
Post a Comment