Takriban watu kumi na moja wa kabila la Pokomo wameuawa katika
mashambulizi mapya ya kulipiza kisasi katika eneo la Tana River,Kusini Mashariki
mwa Kenya.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema alisikia watu wakipiga mayowe
wakati kijiji kimoja kilipokuwa kinashambuliwa na kisha wenyeji kuteketezwa.
Eneo hilo ambako zinaishi jamii za kuhamahama ni kitovu cha mizozo ya ardhi
na maji kati ya jamii za Orma na Pokomo.
Watu wengine kumi walijeruhiwa kwenye uvamizi huo uliotokea usiku wa kuamkia
leo.
Uvamizi huu umetokea baada ya mashambulizi mengine kutokea mwezi jana ambapo
watu 52 kutoka jamii ya Orma wengi wakiwa watoto na wanawake kuuawa kwa
kunyongwa na kuteketezwa kiasi cha kutotambulika.
Ni katika tukio ambalo lilitajwa kuwa ghasia mbaya za kikabila kutokea katika
miaka ya hivi karibuni nchini Kenya. Polisi na viongozi wa kijamii walisaidia
kutuliza hali na kurejesha usalama kati ya jamii hizo mbili lakini hali ya
wasiwasi iimeendelea kutanda.
Licha ya kwamba polisi waliahidi kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo,
viongozi wa eneo hilo wanasema vikosi vya usalama vimeshindwa kuzuia ghasia.
Mbunge wa eneo hilo, Danson Mungatana amewashtumu maafisa wa usalama kwa
kushindwa kuchukua hatua za kuwalinda wananchi licha ya kufahamu mapema kwamba
mashambulio yatatokea.
Jamii hizo mbili za Pokomo na Orma, zimekuwa zikizozana kuhusu matumizi ya
ardhi na maji ambazo ni rasilimali adimu.
Wapokomo ni wakulima ambao hukuza chakula kando ya mto Tana wakati jamii ya
Orma wakiwa wafugaji wa kuhamahama.
|
No comments:
Post a Comment